Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 05:26

Afisa polisi mzungu ashitakiwa kutokana na kifo cha Mmarekani mweusi


Derek Chauvin, afisa wa zamani wa polisi wa Minnepolisi akimwekea goti George Floyd wakati wa kumkamata.
Derek Chauvin, afisa wa zamani wa polisi wa Minnepolisi akimwekea goti George Floyd wakati wa kumkamata.

Afisa wa zamani wa polisi anaeonekana katika video goti lake likiwa shingoni mwa Mmarekani mweusi George Floyd, kabla ya mtu huyo aliyekuwa amefungwa pingu chini ya ulinzi kufariki siku ya Jumatatu amefunguliwa mashtaka ya mauaji na kumuua mtu bila ya kudhamiria.

Mwanasheria wa wilaya ya Hennepin, Mike Freeman ametangaza kwamba Derek Chauvin amefunguliwa mashtaka ya mauaji na shitaka la kumuua mtu bila kudhamiria.

Mapema Ijumaa, kamishna wa Idara ya Usalama wa Raia, wa jimbo la Minnesota John Harrington, aliwaambia waandishi wa habari Chauvin alikamatwa bila ya kufahamu sababu halisi ya uamuzi huo.

Tim Walz, Havanna wa Minnesota
Tim Walz, Havanna wa Minnesota

Gavana wa Minnesota mdemokrat, Tim Walz ameomba kuwepo na utulivu, alipokuwa anaidhinisha amri ya kuwapeleka walinzi wa usalama wa taifa kufuatia ombi la meya wa Minneapolis.

Amesema hawezi kuruhusu wizi na uharibifu kuendelea. Na kusema pia hawezi kukubali ghasia hizo kuwapoteza shabaha muhimu ambayo ni kushughulikia kifo kilichotokea na mvutano uliyopo.

Maandamano yaliyoanza kwa amani Alhamisi jioni mjini Minneapolis yaligeuka kuwa ghasia wakati wa usiku na kufikia saa nne hasira ziliongezeka katika mji huo na mji pacha wa St Paul.

Wadadisi wa mambo wanasema hasira ziliongezeka baada ya mwanasheria mkuu wa jimbo la Minnesota, Erica MacDonald kuzungumza na waandishi habari Alhamisi jioni na kutangaza kwamba uchunguzi unafanyika bila ya kutaja suala la kukamatwa kwa polisi wanne waliohusika na kifo cha Flyod siku ya Jumatatu.

Muandamanaji abeba bango huku majengo yakiteketea Minneapolis
Muandamanaji abeba bango huku majengo yakiteketea Minneapolis

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari polisi na wazima moto waliondoka kutoka kituo hicho ambacho polisi wanne wazungu waliohusika na kifo cha Floyd wanasemekana walikuwa wakifanya kazi. Kuondoka kwao ndio kulisababisha waandamanaji kuingia ndani na kutia moto.

Meya wa jiji hilo Jacob Frey aliyetangaza hali ya dharura aliitisha mkutano Ijumaa alfajiri na kujitetea kutokana na uamuzi wake kuwataka polisi kuondoka kutoka kituo hicho kwa ajili ya usalama wao.

“Mapema jana jioni baada ya kupata habari muhimu kutoka mkuu wa polisi Arradondo na baada ya kuzunguza nae mara kadhaa kuhusu hali inavyoendelea katika kituo hicho cha polisi ilidhihirika wazi kwamba kuna kitisho cha kweli kwa usalama wa polisi sote na raia na ilikua muhimu kuchukuwa uamuzi kuwaondoa. Jengo hilo hauwezi kuwa muhimu zaidi kuliko maisha ya maafisa na raia,” amesema meya Frey

Frey aliendelea kusema ingawa kuna uchungu na hasira, jambo ambalo anafahamu fika, lakini haikubaliki ghasia na wizi kuendelea. Anasema majengo hayo na maduka ni mahala wakazi wa mji huo wanayahitajia sana.

Waandamanaji ndani ya dula la Target kufuatia maandamano ya Minneapoilis
Waandamanaji ndani ya dula la Target kufuatia maandamano ya Minneapoilis

Hata hivyo wakazi wa mji huo wamekuwa wakieleza hasira zao, baadhi wakifahamu yanaotokea lakini wengine wengi wakidai wamechoshwa na unyanyasaji wa polisi na lazima hatua zichukuliwe.

George Farmah mwandamanaji mjini Minneapolis anasema ghasia hizo zinabidi kuwa ni funzo.

"Tumejaribu kwa njia ya amani, tumejaribu kupiga goti, lakini hakuna kilichobadilika. Hivi sasa haya yanatokea, mara nyingine, polisi akijaribu kufanya jambo lolote atafikiria kwanza mara mbili," amesema Farmah.

Rais Donald Trump katika ujumbe wa Tweet Alhamisi usiku, alishambulia uongozi wa mji huo wa Minneapolis kwa kushindwa kurudisha utulivu na kutishia kupeleka walinzi wa usalana au jeshi.

Aliandika “siwezi kukaa kimya na kuona yanayo tendeka katika mji muhimu wa Marekani wa Minneapolis. Ukosefu wa uongozi. Ikiwa meya wa mrengo mkali wa kushoto hawezi kukabiliana na matatizo yake basi nitapeleka walinzi wa usalama wa taifa kufanya kazi inayohitajika.”

Mbunge anaewakilisha jimbo hilo katika bunge la Marekani Ilhan Omar anaendelea kutafuta njia ya uwiano na muelewano.

Anasema, “inavunja moyo kutizama kile kinachotokea usiku kutizama mji ukiteketea. Inasikitisha pia kufahamu kwamba hasira na tafrani inyowajaa watu rohoni hadi kufikia hali hii ya hatari. Kwa hivyo inabidi tutafute njia ya uwiano hapa. Inatubidi tuweza kuandamana kwa amani lakini pia kufanya kazi ili kila mtu amlinde mwenzake," amesema Omar.

Maandamano yamefanyika pia katika miji mingine mikuu ya Marekani kuanzia Chicago, Los Angeles, New York, Columbus na kwengineko kudai haki itendeke na maafisa polisi waliohusika kukamatwa.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG