Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 11:42

Kumbukumbu ya George Floyd : Maandamano siku ya 13 yafanyika kwa amani Marekani


Waandamanaji Jumamosi Juni 6, 2020, wakiwa karibu na White House mjini Washington, DC wakilaani kifo cha Mmarekani Mweusi wakati akishikililwa na polisi Minneapolis, Minnesota. (AP Photo/Jacquelyn Martin)
Waandamanaji Jumamosi Juni 6, 2020, wakiwa karibu na White House mjini Washington, DC wakilaani kifo cha Mmarekani Mweusi wakati akishikililwa na polisi Minneapolis, Minnesota. (AP Photo/Jacquelyn Martin)

Maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa Marekani kwa ajili ya kudai usawa na haki kwa watu wa rangi zote yamefanyika kwa siku ya 13 mfululizo Jumapili katika miji mbali mbali kwa amani ukilinganisha na yale yaliyokuwa na ghasia wiki moja kabla.

Wakati huo huo washauri wa white house wamesema Rais Donald Trump anatarajiwa kulihutubia taifa juu ya suala la ubaguzi baada ya kukosolewa vikali kutokana na pendekezo lake wiki iliyopita kutaka kupeleka wanajeshi kuzima ghasia na maandamano hayo.

Maandamano yalifanyika Washington, Los Angeles na New York Los ambako maelfu ya watu walijitokeza kudaia haki na usawa kwa wote, pamoja na kushinikiza kuwepo mageuzi katika idara za polisi.

Hayo yakiendelea wakuu wa zamani wa jeshi wamekuwa wakijitokeza kumkosoa vikali Rais Donald Trump kwa namna alivyoshughulikia maandamano hayo na hasa kutaka kutumia jeshi kuyazima maandamano hayo, hali ambayo ni nadra kutokea.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na mkuu wa zamani wa majeshi ya Marekani Colin Powell ni miongoni mwa waliomkosoa rais Jumapili pamoja na Mkuu wa zamani wa jeshi Jenerali Martin Dempsey.

Martin Dempsy mkuu wa zamani wa majeshi Marekani amesema: "Nilifikiria kwamba kutokana na hali ya ghasia na hatari ambayo inaweza kuleta athari mbaya katika uhusiano kati ya wanajeshi na raia wa Marekani niliona ni afadhali nitoe maoni yangu.

Washauri wa rais wanamtetea kwa kusema kwamba amri yake ya kuwapeleka walinzi wa usalama wa taifa ndio ilichangia katika kusitisha ghasia.

Hata hivyo wanaharakati wanasema kukamatwa kwa polisi wote wanne waliohusishwa na kifo cha Geoge Floyd ndio iliyosababisha ghasia kusita.

Naye rais wa zamani Barack Obama alizungumza kwa mara ya pili wiki iliyopita alipokuwa anashiriki katika ghafla ya kuwapongeza wanafunzi wanaohetimu vyuo vikuu mwaka huu ambao hawawezi kusherehekea kutokana na janga la corona.

Barack Obama rais wa zamani wa Marekani amesema : "Mnapo jitayarisha kuanza maisha meya inabidi kukumbuka kwamba tunahitaji kufanya mambo yawe mazuri zaidi. Tukumbuke kwamba ustawi wetu binafsi unategemea ustawi katika jamii tunaoishi. Kwa hiyo yanyotokea sasa iwe ni wito wa mwamko kwenu."

Maandamano ya mwishoni mwa wiki yalipata nguvu kutokana na kushiriki kwa wasanii mbali mbali na wachazeji mashuhuri wa mpira wa kikapu, NBA, na American Football, NFL, pamoja wakiunga mkono wito wa kupatikana mageuzi na usawa wa rangi katika fani zote za maisha hapa Marekani.

Wafanyakazi wa afya wa New York walishiriki pia katika maandamano hayo, wakitaka mageuzi kufanyika katika huduma za afya zinazotolewa kwa watu wa tabaka mbali mbali.

Muandamanaji mfanyakazi wa huduma za Afya : "Namna watu weusi na namna walatino na namna watu wa tabaka la chini wanavyotendewa na huduma duni wanaopatiwa katika afya kulinganishwa na wengine na matokeo mabaya ya afya yanayowakabili. Inabidi kubadilishwa."

Mbali na maandamano ya hapa Marekani mandamano yaliendelea katika miji kadhaa ya Dunia ikiwa ni pamoja na Budapest, Paris, Sau Paulo Brazil hadi Sydney Australia.

Katika baadhi ya maandamano hayo watu walikuwa wanawaunga mkono waandamanaji wa Wamarekani na wengine wakidai pia kukomeshwa ubaguzi na utumiaji nguvu wa polisi katika nchi zao kama huko Mexico, Haiti na Brazil.

Hayo yakiendelea kulikuwa na ibada ya maombolezi ya George Floyd katika jimbo alikozaliwa la North Carolina siku ya Jumamosi na maziko yake yamepangwa kufanyika kesho huko Houston alikokulia. Kifo chake ndicho kilichochochea maandamano haya ya kutaka mageuzi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG