Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 17:33

Kimbunga Fiona chapiga Puerto Rico, chaharibu miundombinu ya umeme


Kimbunga Fiona chawasili Puerto Rico.
Kimbunga Fiona chawasili Puerto Rico.

Kimbunga Fiona kimepiga katika kisiwa cha Puerto Rico, kikiharibu miundombinu ya umeme katika eneo la kisiwa hicho cha Marekani na kuongezeka kwa hofu ya “balaa ya mafuriko.”

Kimbunga hicho kinatarajiwa kusababisha mvua zaidi ya sentimita 64 katika baadhi ya sehemu za kisiwa hicho katika kanda ya Caribbean.

Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kimbunga chenye makao yake Miami kilisema katika taarifa yake kuwa Fiona imewasili katika ufukwe wa pwani ya kusini magharibi, karibu na Punta Tocon, majira ya saa tisa na dakika ishirini saa ya eneo hilo Jumapili.

Pepo zilikuwa zinavuma kwa kasi inayokadiriwa kuwa kilomita 140 kwa saa, ikifanya Fiona kuwa ni kimbunga cha daraja la kwanza katika kipimo cha Saffir-Simpson cha kupima ukubwa wa kimbunga.

Kampuni ya nishati ya LUMA [[ lumapr.com]], inayoendesha ugawaji umeme kwenye kisiwa hicho, iliandika katika tovuti yake kuwa “kutokana na ukubwa na kiwango cha kukatika umeme, na pia athari zinazoendelea kujitokeza za kimbunga Fiona, kurejesha umeme kutachukua siku kadhaa.” Kampuni hiyo, hata hivyo, imesema ilikuwa na timu yake, vifaa, na rasilmali kuweza kukabiliana na tukio hili.”

Wakati huo huo, ndege katika uwanja mkuu wa ndege zimesitisha safari na bandari zimefungwa kutokana na dharura ya hali ya hewa. Mapema kabla ya kuwasili kimbunga, baadhi ya wakazi walikwenda kutafuta hifadhi sehemu nyingine wakiondoka majumbani mwao.

Mapema Rais wa Marekani Joe Biden ameidhinisha kutangazwa hali ya dharura kwa Puerto Rico, kulingana na Shirika la Usimamizi wa Dharura la Serikali Kuu (FEMA). Taarifa yake ilisema msaada wa dharura wa serikali kuu umetolewa kwa ajili ya Puerto Rico na kuwa FEMA imepewa idhini ya kuratibu juhudi zote za msaada wa maafa kuweza kupunguza athari ya dharura hiyo inayoendelea.

Fiona imepiga baada ya miaka mitano ya janga la Kimbunga Maria kilichoharibu Puerto Rico kama kimbunga kikubwa. Maria kilikuwa ni kimbunga chenye nguvu sana kilichopiga kisiwa hicho baada ya takriban miaka 90 kilipowasili katika fukwe zake Septemba 2017.

Watabiri wa hali ya hewa pia wanasema Fiona inaelekea huko magharibi ya Puerto Rico katika nchi ya Dominican Republic, ambapo tahadhari ya kimbunga na ufuatiliaji wake unaendelea. Watabiri wanatahadharisha kutokea balaa ya mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo hayo.

XS
SM
MD
LG