Darzeni ya watu Marekani wanahofiwa kufa baada ya mfululizo wa vimbunga kutokea Ijumaa usiku katika majimbo kadhaa ya Marekani, na kusababisha uharibifu mkubwa kutokana na hali ya hewa inayotokea sana katika majira ya Spring.
Gavana wa jimbo la Kentucky, Andy Beshear alikiambia kituo cha televisheni cha WLKY kwamba takriban watu 50 huenda wamefariki na kuongeza kuwa anatarajia idadi hiyo kuongezeka. Beshear alitangaza hali ya dharura na ametoa wito kuwekwa walinzi wa kitaifa wa Kentucky na kupeleka polisi wa serikali ya jimbo.
Huko Edwardsville, polisi wa jimbo la Illinois, walisema katika taarifa kwenye Facebook kwamba hali mbaya ya hewa imesababisha tukio la kuporomoka kwa sehemu ya jengo kwenye ghala ya Amazon, na operesheni za uokoaji zinaendelea.
Kimbunga pia kilipiga nyumba ya kuhudumia wazee huko Monette, kaskazini mwa Arkansas, lakini kiwango cha majeruhi hakijafahamika mara moja. Maafisa walisema vimbunga vilihamia angalau kwenye majimbo matano ya Marekani, ya Arkansas, Illinois, Kentucky, Missouri na Tennessee.