Kimbunga cha Emnati, kinachoelekea Madagascar kinatarajiwa kupiga kisiwa hicho kuanzia jioni ya leo kikiwa na upepo unaokwenda kwa kasi za hadi kilomita 170 kwa saa, idara ya hali ya hewa ya serikali ilisema, na kuwa dhoruba kubwa ya nne kukumba kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi katika mwezi mmoja.
Ofisi ya Kitaifa ya masuala ya dharura na Usimamizi wa Maafa ya Madagascar ilisema karibu watu 275,000 walikuwa kwenye njia ya kimbunga hicho. Maelfu ya watu tayari wamekosa makazi katika msimu wa kimbunga wa mwaka huu.
Ofisi ya taifa ya hali ya hewa ilisema katika taarifa yake kwamba kimbunga hicho kingewasili katika pwani ya mashariki ya kisiwa hicho Jumanne jioni, kuendelea kupitia nyanda za kati, na kuelekea baharini sehemu za magharibi katika pwani ya Msumbiji siku ya Jumatano.
Kisiwa bado kina kabiliana na hasara kubwa kutokana na athari za Kimbunga cha Batsirai, kilichopiga Februari 5, na kuua watu 124 na kuharibu nyumba za watu 124,000. Takriban watu 30,000 zaidi walipoteza makazi yao.