Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 21:06

Kenya kuchunguza maisha ya raia kupitia mitandao ya kijamii


Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini Kenya (KRA) imetangaza kuwa inaanza kuchunguza mwenendo wa maisha ya raia wa nchi hiyo kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya kidijitali ili kubaini iwapo mapato yao yanalipiwa ushuru.

Mamlaka hiyo inasema kuwa raia wengi wa Kenya wamekuwa wakibandika picha zinazoonyesha magari ya kisasa na nyumba za kifahari lakini wanakwepa kulipa ushuru.

Mfumo huo wa mpya wa halmashauri ya kukusanya ushuru nchini Kenya, kwa wafuatiliaji wa masuala ya uchumi unaonekana kama lengo la kuimarisha mapato ya halmashauri hiyo ambayo yamekuwa chini kwa muda mrefu.

Kamishna Mkuu wa mamalaka hiyo James Githii Mburu, wiki hii amevieleza vyombo vya habari nchini Kenya kuwa maafisa wa KRA sasa watatumia muda wao mwingi kuchungulia mwenendo wa maisha ya raia wa Kenya kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya kidijitali kama vile Facebook, Instagram na Snapchat kutathmini iwapo viwango vyao vya mtindo wa maisha vinaendana sambamba na jukumu lao la kulipa ushuru.

Afisa huyo ananukuliwa akieleza kuwa raia wengi wa Kenya wamekuwa wakibandika picha za nyumba na magari ya kifahari, kushiriki burudani na kubugia vileo vya bei ya juu lakini likija jukumu la kulipia ushuru wanakwepa au wanalipia kiasi kidogo kisichoafiki mtindo wa maisha.

Kutokana na taarifa ya maandishi ya shirika hilo kwa vyombo vya habari Jumatano, KRA limeeleza kuwa raia wa Kenya wameanza kujitokeza kuelezea hali zao za mapato na kutafuta mbinu muafaka za kujisajili kwenye mfumo wa ulipiaji ushuru, siku moja tu baada ya kuonesha nia ya kuwachungulia raia wa Kenya kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, raia wa Kenya, kupitia mitandao hiyo, wengine wameonyesha kutoridhishwa na hatua hiyo na kkusema haitekelezeki.

KRA linawataka wanamitindo, watu wengine binafsi na maarufu wanaoishi maisha ya kifahari kwenye mitandao ya kijamii kuwa sehemu ya raia wa Kenya wanaolipia mapato yao ushuru. Aidha, linaongeza kuwa ndani ya mipaka yake ya sheria, litatumia uchunguzi wa mitandao ya kijamii kati ya mifumo mingine ya ufuatiliaji wa kodi ya kiteknolojia kuhakikisha kuwa linaafikia malengo yake kila mwaka.

Charles Karisa, mchumi na mtaalam wa sheria za ushuru anaeleza kuwa KRA litakuwa na kibarua cha ziada kutimiza na kuafikia mfumo huo.

“Huenda ikapata wakati mgumu kuthibitisha kwamba mtu ambaye anaishi maisha ya kifahari. Kwa mfano, je hiyo gari aliyopiga picha nayo ama nyumba ni mahali anakoishi na wataweza kuthibitisha kuwa vitu vile ni vyake. Kwahiyo changamoto ipo kwa serikali ama KRA kutafuta mbinu mbadala kkuhakikisha kwamba wanaweza kuthibitisha vitu vya kifahari vinamilikiwa na huyo mhusika,” ameongeza Karisa.

Mwezi wa Oktoba, KRA ilitangaza kukusanya ushuru wa zaidi ya shilingi bilioni 154.3 na kuzidisha kiwango ilichojiwekea cha shilingi bilioni 142.3 ikiwa ni rekodi nzuri ya zaidi ya asilimia 108.5%, lakini je, KRA ina mfumo unaolielekeza kuchunguza mtindo wa maisha ya watu kwenye mitandao ya kijamii?

Karisa anasema “KRA imepewa madaraka katika kitengo cha Tax Procedures Act, kwahiyo kina nguvu ya kumuita mtu yeyote na kumhoji kujua hali yake.”

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa imeanza mwaka mpya wa fedha kwa kushuhudia kupita kwa kiwango chake cha makusanyo ya ushuru kati ya Julai-Septemba kwa zaidi ya shilingi bilion 15, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 30.

IMETAYARISHWA NA KENNEDY WANDERA, NAIROBI.

XS
SM
MD
LG