Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 19:48

Wahudumu wa Afya Kenya hawana vifaa kinga vya kutosha dhidi ya COVID-19


Aina ya vifaa kinga dhidi ya COVID-19.
Aina ya vifaa kinga dhidi ya COVID-19.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu, Human Rights Watch, katika ripoti yake mpya limesema kuwa serikali ya Kenya imeshindwa kutimiza ahadi yake kuwasaidia wahudumu wa afya walio katika mstari wa mbele kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Human Rights Watch linadai kuwa kushindwa huko kumewaweka wahudumu hao wa afya nchini Kenya kwenya hatari inayoweza kuepukika iwapo serikali ingechukua hatua za haraka kuwalinda dhidi ya athari ya virusi hivyo.

Shirika hilo linadai kuwa, Kenya licha ya kuwekeza rasilimali nyingi katika vita dhidi ya virusi hivyo, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imeshindwa kuwapa wahudumu wa afya vifaa vya kujinga dhidi ya ugonjwa huo.

"Utepetevu wa Kenya kuhusu usalama na mahitaji ya wahudumu wa afya katikati ya janga hili haukubaliki kabisa," amesema Otsieno Namwaya, mkurugenzi wa Afrika Mashariki katika Human Rights Watch.

"Serikali ya Kenya inapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wahudumu wa afya walio katika safu ya mbele ya mapambano dhidi ya Covid-19 wana uwezo wa kufanya kazi katika mazingira ambayo hayatawaweka katika hatari isiyo ya lazima," afisa huyo ameongeza.

Kati ya Machi na Julai 2021, Human Rights Watch linasema kuwa limewahoji wahudumu wa afya wa serikali 28, pamoja na wauguzi 14, madaktari 7 na maafisa wengine wa ngazi ya juu katika wizara ya afya na vile kutumia hati za serikali, ripoti na nakala za magazeti katika ripoti hii, kubaini utepetevu huu unaotajwa katika ripoti yake.

Wahudumu wa afya walionukuliwa katika ripoti hii wanaeleza Human Rights Watch kuwa hawakuwa na vifaa kinga(PPEs), maski, glavu, na mavazi mengine ya kujikinga wakati wa kuwahudumia wagonjwa na wakati serikali ilipotoa agizo la kusambazwa vifaa hivyo, havikuwa vya kutosha. Pia wananukuliwa wakieleza kuwa hawakupewa mafunzo ya kutosha kuwatibu wagonjwa kwenye wodi, hii ikidhoofisha uwezo wao wa kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Utafiti wa Human Rights Watch unaonesha kuwa serikali ya Kenya haikutimiza ahadi yake ya kutoa marupuru ya kufanya kazi katika mazingira magumu kwa wahudumu wa afya nchini humo, haikuwezesha wahudumu hao kupata huduma bora na nafuu wanapolazwa hospitalini wakati wameambukizwa na virusi hivyo na pia kushindwa kulipia gharama ya mazishi kwa wahudumu wa afya waliofariki wakiwa mstari wa mbele kupambana na virusi hivi vinavyoendelea kuitikisa dunia.

Kwa mujibu wa ripoti hii, Human Rights Watch linaeleza kuwa wahudumu wa afya waliohojiwa walisema kuhisi kufanya kazi kupita kiasi, kuwa na msongo wa mawazo wanapotekeleza majukumu hayo na vile hawakuhisi kuungwa mkono na serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona, "tulikuwa tukilipwa shilingi 10,000 za Kenya [$100] kwa mwezi, ambazo hatukupata kwa miezi sita," alisema muuguzi mmoja.

"Serikali haikutupatia marupurupu ya kufanya kazi katika mazingira magumu, hakuna bima ya afya, hakuna PPE, lakini tuliwekwa kwenye vyumba vyenye mahitaji ya dharura ambapo tulikuwa katika hatari zaidi,"anaeleza mhudumu huyo wa afya aliyekuwa miongoni mwa wahudumu wa afya wasiofika 1,000 walioajiriwa na serikali, kwa mujibu wa Human Rights Watch, kupambana na wimbi jipya la virusi hivyo.

Human Rights Watch linasema liliandikia barua Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe kujibu madai ya wahudumu wa afya walionukuliwa katika ripoti hii, lakini hakujibu ila afisa wa sheria katika wizara hiyo alieleza kuwa wizara haiwezi kutoa maelezo kuhusu ripoti hii.

Msemaji wa serikali ya Kenya Cyrus Oguna hakujibu ombi la VOA kuhusu madai haya yalionakiliwa katika ripoti ya Human Rights Watch.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya

XS
SM
MD
LG