Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 09:44

Kenyatta akataa uamuzi wa ICJ kuhusu mpaka kati ya Kenya na Somali, Farmajo airidhia


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kulia) na mwenzake wa Ethiopia Mohamed Abdullahi Farmajo.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kulia) na mwenzake wa Ethiopia Mohamed Abdullahi Farmajo.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amesema kwamba serikali yake haikubaliani kamwe na uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, kuhusu mpaka wa majini, kwenye bahari Hindi, kati yake na Somalia, huku naye Rais wa Somalia Mohamed Abdulahi Farmajo akimtaka atosheke na uamuzi huo.

Kupitia taarifa, Kenyatta alisema kwamba uamuzi huo utachochea uhasama kati ya nchi hizo mbili, akiongeza kwamba ICJ ilikataa kutoa nafasi ya usuluhishi kwa mamlaka za kieneo, zilizo na uwezo wa kutatua mgogoro huo.

"Sina nia ya kuvunja kiapo changu cha kulinda mipaka yetu na nitafanya kila liwezekanalo kama amiri jeshi mkuu kuhifadhi ardhi yetu na kumkabidhi rais atayefuata baada ya muhumla wangu kukamilika chini ya mwaka mmoja kuanzia sasa," Kenyatta alisema.

Taarifa ya Kenyatta, ambaye alikuwa mjini New York, Marekani, kwa ziara rasmi, ilijiri muda mfupi baada ya Rais Mohamed Abdulahi Farmajo wa Somalia kutoa wito kwa Kenya "kuheshimu mikataba ya kimataifa."

Rais Farmajo alisema kwamba nchi yake imerithishwa na uamuzi huo na kuitaka Kenya kutosheka nao.

"Katika kuheshimu sheria na mikataba ya kimataifa, serikali ya Somalia inasema wazi kwamba inakubaliana na uamuzi wa mahakama na tunatarjia nchi jirani ya Kenya kukubaliana na sheria za kimataifa na kushau azma yake ambayo ina misingi ya kupotosha," alisema kupita runinga ya kitaifa.

Kauli za viongozi hao wawili zilifuatia uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo Alhamisi, mjini The Hague, Uholanzi, na kuipatia Somalia umiliki, wa sehemu kubwa ya eneo lililokuwa linazozaniwa.

Mapema Jumanne, mahakama hiyo ilitoa uamuzi ambao kwa kiwango kikubwa unaunga mkono madai ya Somalia katika kesi yake na Kenya kwenye eneo la Bahari ya Hindi, linalozusha ugomvi kati ya nchi hizo mbili.

Mahakama hiyo ilipendekeza ramani mpya, ikigawa sehemu yenye ugomvi, tofauti na jinsi nchi hizo mbili zilivyotarajia.

Jopo la majaji 14 lilisema kwamba Kenya haijatoa ushahidi wa kutosha kwamba Somalia ilikuwa imefikia makubaliano ya namna mpaka wa sasa ulivyochorwa.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo imegawa sehemu inayogombaniwa na hivyo Kenya kupoteza sehemu ya eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita 100,000 mraba.

Uamuzi wa mahakama kwa kiasi kikubwa umeonekana kufurahisha Somali katika kesi ambayo imeonekana kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia kati ya majirani hao wawili.

Sehemu yenye mzozo inaaminika kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.

Kenya inasisitiza kwamba msitari uliochorwa kuelekea mashariki kutoka eneo lililo karibu na Lamu, ambapo kuna mpaka wa Kenya na Somalia, ndio mpaka halisi unaotambuliwa.

Somalia kwa upande wake ilikuwa inasisitiza kwamba mpaka wake unastahili kuwa mstari mstatili jinsi mpaka wake wa ardhi ulivyo

Nchi hizo mbili zilikubaliana mwaka 2009 katika mazungumzo yaliyoungwa mkono na umoja wa mataifa, kusuluhisha mzozo wao wa mpakani kwa njia ya mazungumzo.

Lakini miaka 5 baadaye, Somalia ilielekea katika mahakama ya ICJ baada ya Kenya kuuza leseni za kuchimba mafuta katika sehemu hiyo yenye mzozo kwa kampuni mbili za kimataifa, mwaka 2012.

Wiki jana, katibu wa wizara ya mamo ya nje Macharia Kamau aliishutumu mahakama ya ICJ kwa kile alichokitaja kama mapendeleo na kusema kwamba Kenya haingekubali uamuzi wake.

Mahakama ya ICJ haina nguvu za kutekeleza uamuzi wake.

Gorge Musamali, mchambuzi wa masuala ya usalama katika eneo la Afrika Mashariki na Kati aliiambia idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika kwamba uamuzi mahakama hiyo wa Alhamisi huenda ukapelekea changamoto zaidi za kiusalama kwenye eneo husika.

"Kuna haja ya jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kutafuta suluhisho kwa mgogoro huu kwa sababu tayari tumeshuhudia hali ya taharuki kati ya nchi hizo mbili," alisema.

-Mwandishi wa VOA Kennes Bwire alichangia ripoti hii

XS
SM
MD
LG