Rais wa Marekani, Joe Biden atamkaribisha rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Alhamisi katika ziara ya kwanza ya kiongozi wa Afrika kufika White House toka Biden aingie madarakani.
Mkutano huo utakuwa ni sehemu ya ahadi ya Biden ya ushirikiano na Afrika katika hali ya kuheshimiana na usawa, kwa mujibu wa taarifa ya White House ya Jumanne.
Imeeleza kwamba rais Biden, na rais Kenyatta watajadili mahitaji ya uwazi, na uwajibikaji wa mifumo ya ndani na kimataifa.
Hii ni katika harakati za utawala wa Biden kukabiliana kwa pamoja kuhusu rushwa na kutokuwa na usawa nje ya nchi.
Viongozi hao wawili pia watajadili juhudi za kulinda demokrasia, haki za binadamu, kukuza amani na usalama, pamoja na kuongeza kasi ya ukuwaji wa uchumi, na kukabiliana na matokeo ya tabia nchi.