Mashtaka hayo yanahusiana na kitendo cha Trump kujaribu kinyume cha sheria kutaka kubadilisha kushindwa kwake katika uchaguzi wa 2020 dhidi ya Mdemokrat Joe Biden na kuhamasisha uvunjifu wa amani ili abakie madarakani.
Ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya Marekani, jopo la Baraza la Wawakilishi – wademokrat 7 na Warepublikan wawili wanaompinga Trump - kwa kauli moja wamewataka waendesha mashtaka kumfungulia kesi ya makosa manne dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa Marekani.
Kamati hiyo ilimtuhumu Trump, ambaye aliondoka madarakani mwezi Januari 2021, kwa kuchochea au kusaidia uvamizi, kuzuia mchakato rasmi wa Bunge wakati lilipokutana kurasmisha ushindi wa Biden, njama ya kuihujumu Marekani na hujuma ya kutoa taarifa za uongo.
Hatua za jopo hilo, hata hivyo, hazina amri rasmi na wala kamati hiyo haiwezi kumfungulia Trump mashtaka ya uhalifu.
Lakini tathmini ya kamati hiyo inaweza kutoa msukumo kwa uchunguzi wa uhalifu unaoendelea dhidi ya Trump na wengine ambao tayari unafanywa na mwanasheria maalum Jack Smith, ukisimamiwa na Mwanasheria Mkuu Merrick Garland, pamoja na uchunguzi wa tofauti unaofanywa na mwendesha mashtaka wa jimbo la Kusini la Georgia.
Washirika wa Trump
Jopo hilo pia limepeleka majina ya washirika watano wa Trump – Mark Meadows, Mkuu wa mwisho wa wafanyakazi wa White House kipindi cha utawala wa Trump, na mawakili Rudy Giuliani, meya wa zamani wa New York, John Eastman, Jeffrey Clark na Kenneth Chesebro – kwa uwezekano wa kufunguliwa mashtaka kwa hatua ambazo kamati hiyo imesema Wizara ya Sheria ina uwezo wa kufanya uchunguzi. Wote hao walifanya bidii kubadilisha matokeo ya uchaguzi ili kumweka Trump madarakani.
Kamati hiyo ilisema Kamati ya Maadili ya Baraza la Wawakilishi inalazimika kuchunguza vitendo vya wabunge wanne warepublican, ikiwa ni pamoja na anayetarajiwa kuwa spika ajaye wa bunge, Mwakilishi Kevin McCarthy, kwa sababu ya kukataa kwao kuitikia wito wakufika mbele ya jopo hilo. Warepublikan wengine waliotajwa ni Mwakilishi Jim Jordan, Scott Perry na Andy Biggs.
Kamati inapanga siku ya Jumatano kutoa ripoti kamili na ndefu kuhusu uchunguzi wao uliodumu kwa miezi 18.
Lakini hitimisho moja katika muhtasari wa ripoti hiyo lilisema ushahidi wa jopo hilo “umepelekea kufikia hitimisho la moja kwa moja na lenye nguvu: kuwa kiini kilichosababisha Januari 6 kilikuwa kinatokana na mtu mmoja, Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, ambapo wengi walimfuata. Hakuna chochote kwa matukio ya Januari 6 kingeweza kutokea bila ya Trump.”
Lakini Thompson alisema kuwa Trump “alivunja uaminifu. Alishindwa uchaguzi na alifahamu hilo.” Alisema “kuwajibika” kwa Trump kwa vitendo vyake kunaweza kupatikana kupitia mfumo wa mashtaka ya uhalifu.