Kufuatia tangazao la rais wa zamani wa Marekani Donald Trump wiki iliyopita kwamba atawania tena kiti cha rais kwenye uchaguzi mkuu wa 2024, kundi la wanaharakati wa mrengo wa kushoto limesema kwamba linatafuta uungaji mkono wa kupinga hatua hiyo. Wanaharakati hao wanapanga kutumia kifungu cha katiba kisichojulikana sana, chini ya msingi wa jukumu lake katika uvamizi wa jengo la bunge, uliyofanywa na wafuasi wake Januari 6 mwaka 2021.
Kundi hilo linapanga kutumia kifungo cha 3 cha marekebisho ya 14 ya katiba ya Marekani kinachozuia mtu kushikilia nafasi ya uongozi ya umma, iwapo ameshiriki kwenye vitendo vinavyo hujumu katiba kama kuongoza uasi, au mapinduzi dhidi ya Marekani. Sheria hiyo ilibuniwa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe hapa Marekani vya 1861-1865 ili kuzuia wafuasi wa majimbo yaliokuwa yamejitenga kushikilia nafasi za uongozi.
Hata hivyo ilisitishwa kupitia marekebisho ya bunge ya 1872, lakini baadhi ya wasomi wanasema kwamba huenda ikafufuliwa kufuatia uvamizi wa Januari 6.