Baraza hilo linachukuwa nafasi ya baraza la utawala wa muda la kijeshi, lililoshikilia nchi, baada ya miezi ya maandamano yaliyokuwa na athari mbaya yaliyopelekea kuanguka kwa utawala wa kiongozi wa mda mrefu Omar al-Bashir.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, aliyekuwa kiongozi wa baraza la kijeshi, ameapishwa katika nafasi ya uwenyekiti wa baraza jipya.
Jenerali huyo ataongoza Sudan kwa muda wa miezi 21 katika serikali ya mpito itakayohudumu kwa kipindi cha miezi 39, kabla ya madaraka hayo kurejeshwa mikononi mwa raia.
Abdalla Hamdock, ameteuliwa kuwa waziri mkuu, baada ya jina lake kuidhinishwa na upinzani wiki iliyopita. Kabla ya uteuzi huu alikuwa mchumi katika kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika.
Baraza hilo lina wanawake wawili, akiwemo mwakilishi wa wakristo walio wachache Sudan, na itakuwa na jukumu la kuunda serikali na bunge.
Hatua ya kuundwa kwa baraza la mpito inafuatia makubaliano yaliyosainiwa jumamosi katika hafla iliyohudhuriwa na waakilishi wa nchi kadhaa, na kutoa ishara ya kurejea hali ya utulivu wa kudumu nchini Sudan.
Viongozi wapya wa Sudan wanatarajiwa kushinikiza kuondolewa marufuku kwa Sudan katika umoja wa Afrika kufuatia maandamano mabaya ya mwezi Juni.
Baraza hilo pia litakuwa na jukumu la kutaka Marekani kuiondoa Sudan katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi duniani.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.