Wanachama wa baraza huru pamoja na Waziri Mkuu wa Sudan wanaapishwa Jumatano. Msemaji wa baraza la jeshi linalotawala nchini Sudan aliwaambia waandishi wa habari Jumanne kwamba nchi hiyo ilikamilisha mfumo wa baraza huru lenye wanachama 11 ambao wataongoza serikali ya mpito nchini humo kwa kipindi cha miaka mitatu hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika.
Wiki iliyopita ushirika unaoongoza upinzani ulimteuwa mchumi, Abdalla Hamdok kuhudumu kama Waziri Mkuu katika serikali ya mpito nchini humo.
Mkataba wa kushirikiana madaraka pia unakubali wabunge 300 wa baraza la wawakilishi kuhudumu wakati wa kipindi cha mseto na baraza la mawaziri lenye wasomi.
Changamoto kuu kwa serikali mpya itakuwa matatizo ya kiuchumi kutokana na upungufu wa sarafu ya kigeni na kusababisha maisha magumu kwa wakazi waliochoshwa kusimama mistari mirefu kwa ajili ya kununua mafuta ya gari na mkate.