Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 19:06

Waandamanaji Sudan watumia kampeni ya uasi wa kiraia dhidi ya jeshi


Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, kulia, akutana na ushirika wa vyama vya upinzani ili kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea Sudan katika ubalozi wa Ethiopia mjini Khartoum, Sudan, Juni 7, 2019.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, kulia, akutana na ushirika wa vyama vya upinzani ili kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea Sudan katika ubalozi wa Ethiopia mjini Khartoum, Sudan, Juni 7, 2019.

Viongozi wa maandamano yanayoendelea nchini Sudan wanawahimiza wananchi kushiriki katika kampeni za uasi wa kiraia nchi nzima kuanzia Jumapili kushinikiza jeshi kukabidhi madaraka kwa raia.

Hatua hii imekuja baada ya vitendo vya kinyama vinavyodaiwa kufanywa na jeshi wakati wa kuwaondoa waandamanaji waliyokuwa wamepiga kambi makao makuu ya jeshi.

Uasi wa kiraia ni vuguvugu la raia kukataa kutii baadhi ya sheria, amri au matakwa ya serikali, ambapo hufanyika bila ya kuwepo uvunjifu wa amani.

Tangazo hilo lilitolewa na chama cha wanataaluma wa Sudan, SPA, walioongoza maandamano yaliyopelekea jeshi kumpindua Rais Omar al-Bashir.

Wamesema Jumamosi kuwa harakati za kupinga utawala wa kijeshi zitaanza tena siku ya Jumapili na kuendelea mpaka pale jeshi litakapo salimu amri kukabidhi madaraka kwa raia.

Jeshi linatuhumiwa kuwashambulia waandamanaji na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha mjini Khartoum na hivyo kuvunja matumaini ya kuwepo utawala wa kidemokasia nchini humo.

Vikosi vya usalama viliendesha operesheni maalum ya kuwasambaza waandamanaji waliokuwa wamepiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum. Watu wasiopungua 113 inadaiwa waliuawa kuanzia Jumatatu, Madakatari waliokaribu na waandamanaji wamesema.

Kwa upande wake Wizara ya Afya ya Sudan imetoa idadi ya vifo 61.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa watu wengine zaidi ya 500 walijeruhiwa tangu siku ya Jumatatu na takribani miili 40 imeopolewa kutoka mto Nile mjini Khartoum na kuchukuliwa na vikosi vya usalama.

Viongozi wa SPA wamesema wamekubali Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuwa msuluhishi na amekutana na baraza la kijeshi la Sudan, japokuwa wametoa sharti la kuwepo uchunguzi juu ya vurugu zilizotokea tangu Bashir kuondolewa madarakani.

Vyanzo vya habari nchini Sudan vinasema kuwa waandamanaji wamesema wataendelea na vuguvugu la uasi wa kiraia na hilo litakoma tu pale serikali ya kiraia itakapotangazwa.

Chama cha wanataaluma wa Sudan SPA kimetoa tamko hilo siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kukutana na majenerali wanaotawala na viongozi wa waandamanaji kwa nyakati tofauti katika juhudi za kuanzisha mazungumzo upya baada ya waandamanaji waliopiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi kutawanywa siku ya Jumatatu na matumaini ya mazungumzo kutoweka.

XS
SM
MD
LG