Watawala wa kijeshi wa Sudan walieleza Alhamis kwamba walizuia majaribio kadhaa ya mapinduzi na kwamba baadhi ya maafisa walikamatwa kufuatia ghasia zilizosababisha vifo wakati wa kuwatawanya waandamanaji walioweka kambi nje ya wizara ya ulinzi mjini Khartoum mwanzoni mwa mwezi huu.
Msemaji wa baraza la mpito la kijeshi alieleza kuwa makundi mawili tofauti ya watu walioshukiwa kuhusika katika majaribio ya mapinduzi walikamatwa. Aliongeza kuwa kundi moja lilijumuisha watu watano wakati kundi jingine lilikuwa na zaidi ya watu 12.
Baraza la jeshi lilichukua madaraka kwa njia ya mapinduzi yaliyotokea April 11 wakati maafisa wa jeshi walipomuondoa madarakani na kumkamata Rais wa zamani wa Sudan, Omar al-Bashir baada ya maandamano ya miezi kadhaa dhidi ya utawala wake wa miaka 30.
Uwanja nje ya wizara ya ulinzi mjini Khartoum umekuwa kituo cha maandamano mapya wakati waandamanaji wakitoa wito kwa jeshi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.