Marekani inasema inaukaribisha mkataba wa kushirikiana madaraka uliobuniwa kumaliza miezi kadhaa ya ghasia za kisiasa nchini Sudan.
Mkataba huo uliafikiwa ijumaa kati ya viongozi wanaoandaa maandamano na majenerali wanaotawala nchi baada ya kufanyika mazungumzo ya siku mbili. Marekani imetoa wito wa kukuza kile inachokiita baraza la uhuru lenye mzunguko wa nafasi ya rais kutoka upande wa jeshi na kiraia kwa miaka mitatu.
Wizara ya mambo ya nje Marekani ilisema hii ni hatua muhimu kusonga mbele. Ilielezea matumaini kwamba mkataba utaongoza kuundwa kwa serikali ya muda inayoongozwa kiraia ambayo ndio inasisitizwa na watu wa Sudan.
Nchi ya Sudan imeingia kwenye matatizo ya kisiasa tangu majenerali walipomuondoa Rais wa muda mrefu Omar Al-Bashir kwa njia ya mapinduzi mwezi April kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya umma nchi nzima.