Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 10:46

Amnesty International yasema Kabendera alionewa, hakustahili kununua uhuru wake


Kabendera aachiwa na Mahakama mjini Dar es Salaam.
Kabendera aachiwa na Mahakama mjini Dar es Salaam.

Mara baada ya kuachiwa huru kutoka jela mwandishi wa habari za uchunguzi Eric Kabendera baada ya kulipa faini na fidia ya jumla ya Shs 273 milioni, Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu kimataifa (Amnesty International) ofisi ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika Deprose Muchena ameeleza masikitiko yake juu faini ya fedha kubwa kiasi hicho.

“Wakati habari za kuachiwa kwa Kabendera zimepokelewa kwa furaha baada ya kukaa jela karibuni miezi saba, inashitusha kuona kuwa amelazimishwa kulipa kiwango kikubwa cha faini ili kupata uhuru wake, baada ya kuwa aliwekwa mahabusu kwa uonevu kwa sababu alikuwa anatumia haki yake ya uhuru wa kujieleza.

“Mama yake Kabendera alikufa wakati yeye yuko mahabusu kipindi kifupi baada ya kutoa maombi yake kwa Rais John Magufuli kupitia kituo cha televisheni kwamba amwachie huru mtoto wake.

Taarifa ya Amnesty International inasema kuwa tayari Kabendera ameteseka kwa kiasi kikubwa kwa kutekeleza wajibu wake wa Kiuandishi na alistahili kuachiwa bila masharti yoyote.

"Hakuna haki kabisa katika kile kilichofikiwa mahakamani mjini Dar es Salaam hivi leo," amesema mkurugenzi huyo.

Ameongeza : “Tanzania lazima iache kutumia vibaya sheria zinazotumika kukiuka haki za watu katika kutumia uhuru wao, uhuru wa kujelezea na kupashwa habari, kukusanyika kwa amani na kujiunga na chama wanachotaka."

Shirika hilo limesisitiza kuwa :"Ni lazima nchi ichukue ahadi hadharani kwamba itamhakikishia kila mtu ana uhuru wa kutumia haki zao zote za kibinadamu na kuacha kutumia sababu zinazochochewa na siasa kuwabana wapinzani na waandishi kama Eric Kabendera.”

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG