Kenya inasema msaada huo wa mbolea kutoka Russia utatumiwa kutengeneza tani laki moja za mbolea aina mbali mbali, kisha kuwauzia Wakenya katika mpango unaoendelea wa kuwapa wakulima mbolea kwa bei nafuu.
Akizungumza mjini Mombasa baada ya kuipokea meli iliyobeba shehena ya mbolea, Waziri wa kilimo nchini Kenya Mithika Linturi amesema hatua hiyo itaboresha kilimo na hivyo kuhakikisha usalama wa chakula nchini humo.
“Wakulima wamenunua zaidi ya magunia milioni 2.8 ya mbolea katika majimbo 34 nchini Kenya na mbolea hii tuliyoipokea itatusaidia kuwafikia wakulima zaidi walio katika maeneo mengine nchini humu,”amesema waziri Linturi.
Russia inakusudia kutoa tani laki 3 za mbolea kwa mataifa yanayoendelea duniani kwenye hatua inayolenga kuimarisha usalama wa chakula ulimwenguni.
“Wakati kuna misukosuko duniani, wakulima wadogo wadogo ndio wanaoumia na serikali yangu inajivuna kusaidia kuondoa njaa na kuzuia hasara ya mimea,” amesema balozi wa Russia nchini Kenya Dmitry Maksimychev.
Shehena ya mbolea hiyo bandarini Mombasa imehusisha kemikali za Potash, Urea na NPK ambayo itatumiwa kuzalisha mbolea kutumika kwenye ukulima wa mimea mbali mbali.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limehusika katika kuisafirisha mbolea hiyo kutoka Ulaya huu ukiwa msaada wa kwanza Kenya kupokea kutoka Russia tangu kuzuka kwa vita kati yake na Ukraine.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergei Lavrov nchini Kenya ambako alikutana na rais William Ruto na spika wa bunge Moses Wetangula kabla ya kuelekea nchini Burundi.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Collins Adede, Kenya
Forum