Video zinazopigwa na watu wa kawaida na kupachikwa katika mitandao ya kijamii zilionyesha makundi ya waandamanaji, baadhi wakiwa katika magari na wengi wao wakitembea kwa miguu, wakifurika katika barabara inayoelekea makaburi ya Aichi katika jimbo la Kurdistan mjini Saqez ambako ndio yalikuwa makazi ya Amini.
Mashuhuda wa tukio hilo wamerepoti risasi zilifyatuliwa katika eneo hilo na majeshi ya usalama ya Iran.
Waandamanaji walikuwa wakisikika wakipiga makelele, “Kifo kwa dikteta” kati ya matamko mengine, wakiandamana kukaidi hatua za kiusalama zilizoongezwa katika eneo hilo ikiwa panatarajiwa kuwepo maandamano zaidi Jumatano.
Idhaa ya VOA Persia ilirepoti kuwa waandamanaji pia walikusanyika Tehran, ambako walipiga makelele “Uanguke utawala wa dikteta” na “Usiogope, tuko sote pamoja.”
Amini, msichana wa Kikurdi, alikamatwa na polisi wa maadili katika mji mkuu, Tehran, Septemba 13 kwa madai hakuvaa “ipasavyo” kitambaa cha kichwani – au hijab. Msichana huyo wa miaka 22 alifariki akiwa amezuiliwa polisi siku tatu baadae, huku polisi wakirepoti kuwa alipata shinikizo la moyo. Familia yake inasema mtoto wao hakuwahi kuwa na historia ya tatizo la moyo.
Maombolezo ya kifo yanaadhimishwa katika madhehebu ya Kiislam ya Kishia – kama ilivyo katika tamaduni nyingine – zikipita siku 40 baada ya kifo, ni desturi ya kuonyesha huzuni. Askari wa kutuliza ghasia na wanamgambo wa kikosi cha Basij viliripotiwa kupelekwa huko Saqez na maeneo mengine ya Kikurdi.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti kuwa shule na vyuo vikuu vyote katika jimbo hilo vimefungwa Jumatano kwa sababu ya kile mamlaka ilichosema ni wimbi la mafua makali ya Influenza
Sehemu ya ripoti hii inatokana na taarifa za mashirika ya habari ya AP, Reuters and AFP.