Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekanusha ripoti zinazodai kwamba Tehran inahusika na vita vya Ukraine.
Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesisitiza kwamba mpango wa Iran kuiuzia Russia silaha ni wa kibiashara, ikitiliwa maanani kwamba Iran ni muuzaji mkubwa wa silaha.
Amesema kwamba mataifa mengi yamekuwa yakitaka kununua silaha kutoka kwa Iran kwa sababu silaha zake ni nzuri zaidi.
Raisi hajasema aina ya silaha ambazo nchi nyingi zimetaka kununua kutoka Iran, wala kuzitaja nchi hizo, lakini amedai kwamba kutokana na ubora wa silaha za Iran, maadui wake wana hasira sana kwamba imepata soko kubwa.
Amesema kwamba adui atakasirika hadi afe kwa sababu ya Iran.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanaani, amesema kwamba hatua ya Ufarasa, Ujerumani na Uingereza kutaka ufanyike uchunguzi dhidi yao ni uongo mtupu usiokuwa na msingi wowote, na kwamba Iran “inakataa hatua hiyo kwa njia zote”.
Ukraine imesema kwamba Russia imekuwa ikitumia ndege zisizo na rubani za Iran kutekeleza mashambulizi ya makombora.
Iran imesema kwamba haitasita kutetea maslahi ya watu wake.