Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 12:45

Russia inawaondoa wanajeshi wake Kherson huku wanajeshi wa Ukraine wakikaribia


Wanajeshi wa Ukraine wakiwa wamepanda gari la kijeshi katika kijiji cha Shandrygolovo, karibu na Lyman, Ukraine. Okt 4, 2022
Wanajeshi wa Ukraine wakiwa wamepanda gari la kijeshi katika kijiji cha Shandrygolovo, karibu na Lyman, Ukraine. Okt 4, 2022

Taasisi inayofuatilia vita vya Ukraine - ISW, imesema kwamba Russia imewaondoa wanajeshi wake kutoka mji wa Kherson karibu na mto Dnieper, kutokana na uhakika kwamba wanajeshi wa Ukraine wanakaribia kuingia mjini humo.

Ili kuchelewesha mashambulizi ya Ukraine, wakati wanajeshi wa Russia wakiondoka, Moscow imewaacha wanajeshi wake waliosajiliwa hivi karibuni, na ambao hawana ujuzi wa mapigano katika upande wa pili wa mto huo.

Kulingana na shirika la habari la AFP, Jeshi la Ukraine limesema kwamba wanajeshi wake wameendeela kutekeleza mashambulizi ya kuwajibu wanajeshi wa Russia katika maeneo ya Kherson na Zaporizhzhia.

Maafisa walioteuliwa na Russia kusimamia sehemu ambazo Russia ilizinyakua kimabavu nchini Ukraine, waliwaambia wakaazi wa Kherson kuondoka haraka iwezekanavyo Jumamosi, kwa matarajio kwamba wanajeshi wa Ukraine walikuwa wanakaribia kuingia mjini humo.

Naibu kiongozi wa mji wa Kherson aliyeteuliwa na Russia, Kirill Stremousov, amesema kwamba raia 20,000 wameondolewa Kherson kufikia Jumapili na wamehamia upande wa kushoto wa mto Dnieper.

Amesema kwamba wanajeshi wa Ukraine walikuwa wanajaribu kuanzisha mashambulizi upande wa kulia ambapo kuna wanajeshi wa Russia.

Russia imeudhibiti Kherson tangu Februari

Wanajeshi wa Russia wamekuwa wakiushikilia mji wa Kherson kwa muda wa miezi 8 ya vita hivyo.

Kherson ni mji mkuu wa mkoa wa Kherson, mojawapo ya mikoa 4 ambayo Russia imejiingiza kimabavu kutoka kwa Ukraine na rais Vladimir Putin ametangaza matumizi ya sheria ya kijeshi katika sehemu hizo.

Wanajeshi wa Ukraine walitekeleza mshambulizi mazito dhidi ya wanajeshi wa Russia siku ya Ijumaa katika sehemu kadhaa za Kherson, kwa matayarisho ya kuukomboa mkoa huo kutoka kwa Russia.

Taasisi inayofuatilia vita vya Ukraine ISW, pia imesema kwamba mkakati wa Russia katika vita hivyo, wa kuharibu mfumo wa umeme na maji kwa makombora unaonekana kuwataka wanajeshi wa Ukraine kuacha kupigana na badala yake kutumia kiasi kikubwa cha rasilimali kulinda watu wake na mfumo wake wa nishati.

Mashambulizi dhidi ya mfumo wa nishati yamepelekea kusitishwa kwa utengenezaji wa mbolea katika mojawapo ya viwanda vikubwa vya kutengeneza mbolea, cha Rivneazot, Kaskazini Magharibi mwa Ukraine.

Wanajeshi wa Russia wanazingatia zaidi kujilinda wenyewe

Jeshi la Ukraine limesema Jumapili, kwamba wanajeshi wa Russia kwa sasa wanazingatia zaidi kujilinda, lakini wanatumia makombora kushambulia mfumo wa nishati wa Ukraine katika sehemu kadhaa za mashariki mwa Donbas.

Mikoa tisa yote nchini Ukraine, kuanzia Odesa, kusini magharibi hadi Kharkiv kaskazini mashariki, yameshuhudia mashambulizi ya makombora yanayolenga mifumo muhimu ya nishati katika siku chache zilizopita.

Zaidi ya makombora 125 yameangushwa na Russia katika miji ya Ukraine.

Mashambulizi ya wanajeshi wa Ukraine katika maeneo ya Kherson na Zaporizhzhia yanalenga sehemu ambazo zimeshikiliwa na wanajeshi wa Russia.

Makombora 17 yamevurumishwa na wanajeshi wa Ukraine.

Jeshi la Ukraine limeandika ujumbe wa Telegram kwamba limeharibu ndege zisizo na rubani 14 za Iran zilizokuwa zinatumika kutekeleza mashambulizi yanayoongozwa na Russia.

Magavana katika maeneo mawili ya Russia yanayopakana na Ukraine, katika sehemu ya kaskazini mashariki, wamesema kwamba wameweka uzio wa kijeshi ili kuzuia mashambulizi ya wanajeshi wa Ukraine.

Wanajeshi wa Russia wakiwa wameshika doria nje ya kiwanda cha umeme cha Kakhovka, karibu na mto Dnieper, Kherson, kusini mwa Ukraine. May 20, 2022
Wanajeshi wa Russia wakiwa wameshika doria nje ya kiwanda cha umeme cha Kakhovka, karibu na mto Dnieper, Kherson, kusini mwa Ukraine. May 20, 2022

Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza ndege Ukraine amekamatwa

Kwingineko, maafisa wa usalama wa Ukraine wamesema kwamba wanamzuia mkuu wa kiwanda cha kutengeneza injini za ndege, ambaye amehudumu katika kiwanda hicho kwa muda mrefu sana.

Anashutumiwa kwa kile kilichotajwa kama kushirikiana na Russia kuhakikisha kwamba wanajeshi wa Russia wana vifaa vya ndege za vita.

Viacheslav Bohuslaiev, rais wa kiwanda cha Motor Sich mjini Zaporizhzhia, na afisa mwingine wa ngazi ya juu katika kiwanda hicho, wamefunguliwa mashtaka ya ‘kulisaidia taifa adui.’

Maafisa wa usalama wa Ukraine wamesema kwamba wawili hao wanashutumiwa kwa kushirikiana na kiwanda cha Russia kinachotengeneza silaha, chenye ushirikiano wa karibu sana na Kremlin, kutoa injini za ndege za Ukraine na vifaa vingine vya ndege kwa wanajeshi wa Russia.

Maafisa wa Russia wamesema kwamba wawili hao walitekeleza mpango huo kwa kushirikisha nchi tatu, ili kukwepa vikwazo dhidi ya Russia.

Kiwanda cha Motor Sich, kimekuwa kikitengeneza injini za ndege tangu enzi za muungano wa Sovieti.

Kiwanda hicho kimekuwa kikilengwa na makombora ya Russia katika vita vinavyoendelea Ukraine.

XS
SM
MD
LG