Twitter yaeleza azma ya kumiliki operesheni za TikTok Marekani

Kampuni ya Twitter Inc imewasiliana na mmiliki wa mtandao wa TikTok ByteDance ikionyesha nia yake ya kununua operesheni za mtandao huo unaendeshwa Marekani.

TikTok ni programu au app ya kutumiana picha za video, na watu wawili wanaolifahamu suala hili wameliambia shirika la habari la Uingereza, Reuters, kuhusu nia ya Twitter Inc kutaka kufanya manunuzi hayo.

Hata hivyo hakuna uthibitisho wowote iwapo Twitter itaweza kununua na kuipiku kampuni ya Microsoft Corp na kuweza kukamilisha ununuzi huo katika siku 45 Rais wa Marekani Donald Trump alizowapa ByteDance kufikia makubaliano ya kuuza kampuni hiyo, chanzo kimeeleza Jumamosi.

Taarifa za Twitter na TikTok kuwa katika hatua za awali za mazungumzo na Microsoft ikionekana kama inaongoza katika manunuzi hayo ya programu hiyo ya TikTok inayoendeshwa Marekani iliripotiwa hapo awali na jarida la The Wall Street.

Twitter inamtaji katika soko wa takriban dola bilioni 30, ambayo inakaribia thamani ya rasilmali za TikTok ambazo zitauzwa, na itahitaji kutafuta mtaji zaidi kuweza kulipia manunuzi hayo, kwa mujibu wa chanzo cha habari.

“Twitter itakabiliwa na wakati mgumu kuweza kukusanya fedha za kutosha kununua mtandao wa TikTok unaoendesha shughuli zake Marekani. Haina uwezo wa kukopa kiasi cha kutosha,” amesema Erik Gordon, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Michigan.

“Iwapo Twitter itajaribu kukusanya kikundi cha wawekezaji, masharti yatakuwa magumu. Wadau wake wanaomiliki hisa wanaweza kupendelea uongozi uweke mkazo na uangalizi zaidi katika biashara ambayo tayari wanayo.

Mmoja wa wenye hisa katika kampuni ya Twitter, kampuni ya Silver Lake, inapendelea kusaidia kutoa fedha kudhamini manunuzi haya, chanzo kimoja kimeeleza.

TikTok imekosolewa na wabunge wa Marekani kutokana na wasiwasi wa shughuli zake kuingilia usalama wa taifa kuhusiana na ukusanyaji wa takwimu.

Mapema wiki hii, Trump alizindua makatazo kadhaa katika kufanya miamala na wamiliki wa programu za ujumbe mfupi WeChat na TikTok, na kuongeza mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Trump alisema wiki hii atasaidia juhudi za kampuni ya Microsoft kununua operesheni za TikTok Marekani kwa sharti ya kwamba serikali ya Marekani ipatiwe “kiwango cha kutosha” cha pato hilo. Hata hivyo alisema atapiga marufuku TikTok app hiyo maarufu ifikapo September 15.

Microsoft imesema Jumapili inakusudia kukamilisha mazungumzo kwa ajili ya manunuzi ya TikTok katikati ya mwezi Septemba.