Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:23

Somalia : Mlipuko wa kujitoa muhanga waua tisa na kujeruhi 20


Magari ya kubeba wagonjwa yakiwa katika eneo la tukio la mlipuko karibu na kituo cha jeshi Mogadishu, Somalia, Agosti 8, 2020.
Magari ya kubeba wagonjwa yakiwa katika eneo la tukio la mlipuko karibu na kituo cha jeshi Mogadishu, Somalia, Agosti 8, 2020.

Watu wasiopungua tisa wameuawa na takriban wengine 20 kujeruhiwa Jumamosi katika mlipuko wa bomu lililokuwa ndani ya gari mbele ya mlango wa kuingilia kwenye kituo cha kijeshi mjini Mogadishu, mashahidi na maafisa wa usalama wamesema.

Maafisa usalama wa serikali waliohojiwa na VOA wamethibitisha kuwa nane kati ya wale waliouawa ni wanajeshi wa serikali na wengine ni wanafamilia wa wanajeshi waliokuwa katika kambi hiyo wakati huo wa mlipuko.

“Mjitoa muhanga akiendesha gari lililobeba mabomu aliongeza kasi mbele ya mlango wa mbele wa kituo hicho cha kijeshi lakini walinzi walipiga bunduki kuzuia lisiingie kabla halijalipuka,” Aden Mohamed afisa polisi kati ya watu wa kwanza kufika katika tukio ameiambia VOA.

Sauti ya mlipuko huo ulisikika katika eneo lote, na moshi mweusi ulizagaa hewani.

“Niliona miili ya wanajeshi wasiopungua nane na gari ya huduma ya dharura iliyokuwa ikiharakisha kufika katika eneo la tukio kuwaondoa majeruhi,” shuhuda wa tukio ameiambia VOA kwa sharti jina lake lisitajwe.

Vyanzo vya habari katika hospitali mbalimbali wamethibitisha kuwa watu 20 wengi wao wakiwa wanajeshi wamejeruhiwa katika mlipuko wa leo.

XS
SM
MD
LG