Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 04:50

Facebook wafuta ujumbe wa Trump wakidai unapotosha habari za COVID-19


Rais Donald Trump
Rais Donald Trump

Wakuu wa Facebook wamefuta ujumbe wa Rais Donald Trump kwa kwenda kinyume na sera inayokataza kupotosha habari za virusi vya corona.

Ujumbe huo ulioonyesha picha ya video ya Fox News ambapo Trump anasema watoto “wanakinga asili” dhidi ya virusi hivyo.

Facebook ilisema Jumatano kuwa “picha ya video inajumuisha madai yasiokuwa sahihi kwamba kikundi cha watu wanakinga dhidi ya COVID-19 jambo ambalo linakiuka sera zetu mbalimbali juu ya madhara ya upotoshaji wa taarifa za COVID.”

Saa kadhaa baadae, kampuni ya Twitter ilizuia kwa muda kampeni ya Trump kutuma ujumbe katika akaunti yake, mpaka itakapo ondoa video hiyo yenye utata. Akaunti ya Trump ilituma video hiyo tena.

Kampuni hiyo imesema katika taarifa iliyotolewa Jumatano jioni kuwa ujumbe huo ulivunja kanuni zinazokataza upotoshaji wa COVID.

Wakati ujumbe wa tweet unapovunja kanuni zake, Twitter inawataka watumiaji wa mtandao kuondoa tweet hiyo inayolalamikiwa na inawakataza kutoweka ujumbe wowote mwengine mpaka wafanye hilo.

Twitter kwa ujumla imekuwa inafanya haraka kuliko Facebook katika miezi ya karibuni kuweka ilani kwa ujumbe wote wa rais ambao unakiuka sera zilizowekwa dhidi ya upotoshaji wa taarifa na unyanyasaji.

Hii si mara ya kwanza kwa Facebook kuondoa ujumbe wa Trump, Facebook imesema, lakini ni mara ya kwanza imefanya hivyo kwa sababu inaeneza taarifa potofu juu ya virusi vya corona. Kampuni hiyo imetoa tahadhari kuhusu ujumbe anaotoa.

Utafiti mbalimbali unaeleza, lakini hujaweza kuthibitisha, kuwa watoto ni nadra kuambukizwa kuliko watu wazima na aghlabu wanakuwa na dalili hafifu za maambukizo. Lakini hilo siyo sawa na “kinga kamili” dhidi ya virusi.

Utafiti wa Kituo cha Kuzuia Maambukizi ya Maradhi (CDC) kilichowahusisha watoto 2,500 uliochapishwa mwezi Aprili umegundua kuwa mmoja kati ya watoto watano wenye maambukizi walilazwa hospitali ukilinganisha na watu wazima ambapo mmoja kati ya watatu walilazwa ; na watoto watatu walifariki.

Utafiti huo unakosa takwimu kamili kwa matukio yote ya maambukizi, lakini pia inapendekeza kuwa watoto wengi waloambukizwa hawana dalili zozote, kitu kinachoweza kuwafanya waeneze virusi kwa wengine.

XS
SM
MD
LG