Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:31

Lebanon yaendelea na maombolezi wakati shughuli za uokoaji zikiendelea


Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kulia, akitembelea eneo liloathiriwa na mlipuko katika bandari ya Beirut , Lebanon, Alhamisi Agosti 6, 2020.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kulia, akitembelea eneo liloathiriwa na mlipuko katika bandari ya Beirut , Lebanon, Alhamisi Agosti 6, 2020.

Waokoaji wameendelea Alhamisi kutafuta watu katika vifusi vya majengo mjini Beirut wakati nchi ikiendelea kuomboleza wale wote waliouwawa katika mlipuko mkubwa jumanne katika bandari ya mji mkuu huo wa Lebanon.

Wizara ya afya inasema idadi ya waliopoteza maisha imeongezeka na kufikia 137, pamoja na zaidi ya watu 5,000 kujeruhiwa katika mlipuko huo. Hata hivyo maafisa wanatarajia idadi ya vifo kuongezeka.

Wakati huohuo mamlaka za usalama zinafanya uchunguzi kujua chanzo cha mlipuko, na viongozi wanaangazia zaidi kile kilichoelezwa kuwa ni kemikali ya ammonium nitrate ambayo ilikuwa imehifadhiwa katika ghala kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.

WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza Alhamisi kwamba hospitali tatu za mjini Beirut ziliharibiwa vibaya katika mlipuko na kwa sasa hazifanyi kazi. WHO inaeleza kuwa hospitali mbili zinafanyakazi kwa ufanisi mdogo.

Jumuiya ya kimataifa imetoa rambirambi kwa wote waliopoteza maisha na kutoa misaada kwa watu wa Beirut kwa ajili ya kuwapatia unafuu.

Ufaransa

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron anatembelea Beirut leo kukutana na viongozi wa kisiasa. Ufaransa, mtawala wa zamani wa Lebanon, inatuma madaktari wa dharura, na tani kadhaa za vifaa vya matibabu.

Rais wa Ufaransa

“Katika siku zijazo, tutajipanga kusaidia, Ufaransa na Ulaya kwa ujumla. Ninapanga mshikamano wetu wa Ulaya, na kwa ujumla mshikamano wa kimataifa, na katika saa kadhaa zijazo, Ufaransa itapendekeza mikakati na mijadala na tutakuwa na timu ya usaidizi kwa wananchi na mamlaka pia,” amesema Macron.

Nazo Qatar na Russia zimefungua hospitali za muda pamoja na kupeleka wafanyakazi wa afya, huku Iraq ikipeleka wafanyakazi wake wa afya pamoja na malori yakiwa na dawa. Nayo Tunisia imejitolea kuwarejesha wagonjwa mahospitalini kwa matibabu.

Austalia imesema Alhamisi kwamba itachangia kiwango cha fedha dola milioni 1.4 kwa Beirut, huku Uingereza ikiahidi kuchangia dola milioni 6.6 ya misaada, na Hungary ikieleza kuchangia dola milioni 1.2 kusaidia uokozi na juhudi za kurejesha tena hali ya kawaida.

Marekani kupitia wizara ya mambo ya nje pia imesema Jumatano kwamba Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo alizungumza na Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab kumuhakikishia kwamba Washington ipo pamoja na watu wa Lebanon katika kuwasaidia.

Mike Pompeo amesema :“Kwa niaba ya Marekani, natuma salamu zetu za rambirambi kwa wote walioathirika na mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut. Tuna simama pamoja kusaidia serekali ya Lebanon inayopitia kipindi kigumu. Mtaona Marekani ikitangaza vitu kadhaa vitavyo saidia watu wa Lebanon katika siku za zijazo.”

Darzeni za watu hawajulikani waliko

Dazeni za watu hawajulikani walipo, na inafikia takriban robo milioni ya watu wameachwa bila makazi baada ya mlipuko hue kuvunja majengo na kuharibu samani zilizorushwa mpaka mitaani kupitia madirishani kwenda kilometa kadhaa.

Familia zilikusanyika karibu na bandari kutafuta taarifa za wale wote waliopotea, na kusababisha hasira kubwa dhidi ya mamlaka kwa kuruhusu kiwango kikubwa cha shehena za kemikali zenye kulipuka kuhifadhiwa kwa miaka yote katika sehemu isiyo salama ndani ya ghala la bandari.

Benki ya dunia inaeleza kwamba itafanya kazi na washirika wa Lebanon, kuanzisha mpango wa umma na binafsi kufadhili ujenzi. Haikufahamika kama hiki kitaathiri mazungumzo yaliokuwa mashakani baina ya Lebanon na Shirika la Fedha la Kimataifa.

Lebanon iko katika maombolezi

Waokozi hii leo wameendelea kutafuta watu katika vifusi vya majengo mjini Beirut wakati nchi ikiendelea kuomboleza wale wote waliouwawa katika mlipuko mkubwa Jumanne katika bandari ya mji mkuu huo wa Lebanon.

Wizara ya afya inasema idadi ya waliopoteza maisha imeongezeka na kufikia 137, pamoja na zaidi ya watu 5,000 walio jeruhiwa katika mlipuko. Maafisa wanatarajia idadi ya vifo kuongezeka.

XS
SM
MD
LG