Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 14:53

Maafisa kadhaa wachunguzwa Afrika kusini kwa ufisadi kutokana na zabuni za vifaa dhidi ya virusi vya corona


Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa

Mamlaka ya kupambana na ufisadi nchini Afrika kusini ilisema Jumatu ilisema inachunguza madai ya ufisadi katika utoaji wa zabuni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kupambana na janga la Corona nchini humo.

Serikali inashutumiwa kwa ufisadi mkubwa katika kupambana na janga hilo.

Uchunguzi huo wa mwendesha mashtaka mkuu, unajiri punde tu baada ya wachunguzi kuanza uchunguzi mwingine kuhusiana na ununuzi wa vifaa vya kuwakinga madaktari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona wanapowashughulikia wagonjwa, katika mkoa wa Gauteng, ambao ndio kitovu cha ukuaji wa uchumi wa Afrika kusini.

Rais Cyril Ramaphosa aliingia madarakani kwa ahadi ya kupambana na ufisadi baada ya aliyemtangulia, Jacob Zuma, kuondolewa madarakani na chama chake cha Africa National Congeress – ANC.

Ramaphosa ameahidi kwamba serikali yake itawachukulia hatua kali wote wanaotumia njia zisizofuata sheria wakishirikiana na maafisa wa serikali kupora mali ya uma.

“Hatutaruhusu mali ya uma ambayo imepatikana kwa hali ngumu na walipa ushuru, wafadhili na jumuiya ya kimataifa kutoweka kutokana na ufisadi,” alisema Ramaphosa.

Muungano mkubwa wa wafanyakazi COSATU, na ambao unashirikiana sana na chama kinachotawala cha ANC, umesema katika taarifa ya maandishi kwamba serikali ya Ramaphosa imechukua hatua za haraka kupambana na madai hayo ya ufisadi.

Muungano huo umetaja ufisadi kuwa tishio kubwa la uchumi wa Afrika kusini.

Mwendesha mashtaka ya uma amesema kwamba ofisi yake inachunguza madai ya ufisadi katika mikoa mitatu, ikiwemo kituo cha karantini kinachosemekana kumilikiwa na afisa wa serikali, pamoja na ununuzi wa vifaa vya matibabu kutoka mkoa wa Kwa Zulu Natal.

Hadi tukiandaa ripoti hii, zaidi ya watu nusu milioni walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona nchini Afrika kusini, ikiwa ndio idadi ya juu zaidi Afrika.

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic alliance, kimetaka kikao cha bunge kufanyika kwa haraka kujadili kile kimetaja kwamba “sherehe ya watu kula” inayofanywa na watu kutoka chama kinachotawala cha ANC.

Inaripotiwa kwamba kanuni za kisheria katika utoaji wa zabuni katika ununuzi wa vifaa vya matibabu kwa wagonjwa wa Corona zilivunjwa na zabuni kutolewa kwa ushirikiano wa watu.

Msemaji wa chama cha ANC hakupatikana kwa simu alipotafutwa na shirika la habari la Reuters.

Msemaji wa rais Cyril Ramaphosa Khusela Diko, na afisa wa afya wa ngazi ya juu wa Gauteng wamechukua likizo ya mda baada ya ripoti ya vyombo vya habari kueleza kwamba bwanaye Diko alishinda zabuni ya kununua vifaa vya matibabu kwa serikali ya Gauteng.

Diko na mmewe wamesisitiza kwamba hawajafanya kosa lolote, na afisa huyo wa afya amedai kwamba hakujihusisha na ununuzi wa vifaa hivyo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG