Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 10:57

Mashambulizi ya 1998 Afrika Mashariki: Miaka 22 baadaye, waathirika wasema hawajatendewa haki


Hali ilivyokuwa baada ya shambulizi la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Marekani nchini Kenya mnamo mwaka wa 1998
Hali ilivyokuwa baada ya shambulizi la kigaidi dhidi ya ubalozi wa Marekani nchini Kenya mnamo mwaka wa 1998

Ni miaka ishirini na miwili tangu mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga ubalozi wa Marekani nchini Kenya, na nchini Tanzania kwa wakati mmoja, na kusababisha zaidi ya watu 200 wakiwa wamekufa na maelfu kujeruhuhiwa.

Ni mashambulizi ambayo yametajwa na wachambuzi kama yaliyolitambulisha kundi la kigaidi la Al-Qaeda kwa ulimwengu.

Siku ya Ijumaa maadhimisho yalipangwa kufanyika katika maeneo ya mashambulizi hayo mjini Nairobi, Kenya, ingawa hakukutarajiwa hafla kubwa kwa sababu ya changamoto za janaga la Corona.

Licha ya kwamba mengi yamefanyika tangu mashambulizi hayo kutokea, ikiwa ni pamoja na washukiwa kukamatwa na hata mahakama kuamuru kwamba baadhi ya wahanga walipwe fidia, bado kuna maswali mengi, miaka ishirini na miwili baadaye.

Ilikuwa ni siku ya Ijumaa tarehe saba mwezi Agosti mwaka wa 1998. Kwa wengi mjini Naironi nchini Kenya, na Dar es Salaam, nchini Tanzania, ilikuwa ni kama Ijumaa nyingine yoyote.

Watu walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Lakini ilipofika mwendo wa saa nne na nusu asubuhi, kila kitu kilibadilika.

Milipuko mikubwa ilisikia kwenye makutano ya barabara za Moi Avenue na Haile Salasie Avenue. Lilikuwa ni tukio la kutisha, ambalo halikuwa limeshuhudia katika historia ya Kenya.

Jengo la ubalozi wa Marekani nchini Kenya lilikuwa limelipuliwa, pamoja na majengo mengine yaliyolizunguka.

Dakika chache baadaye, kilomita 832 kutoka Nairobi, hali ilikuwa ni hiyo hiyo kwenye ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania.

Hali ya taharuki ilitanda. Mamia ya watu wakafa na maelfu kujeruhiwa. Mamia walionekana wakitoroka, baadhi wakiokolewa na kukimbizwa hospitalini, huku nguo zao zikiwa na damu.

Vifusi vilitapakaa kila pahali, watu wakijaribu kuelewa ni nini hasa kilikuwa kimetokea.

Ali Mwadama ni mmoja wa wale walionusurika lakini wakiwa na majeraha mabaya.

"Sijaona kitu kama hicho maishani mwangu. Taharuki ilitanda. Hatukujua nini kimetokea ila tulijipata na majeraha mabaya...damu ilikuwa kila pahali. Hadi leo, nikisikia mlipuko wa aina yoyote, huwa natoroka," alisema mwadama akizungumza na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika.

Mwishowe, watu 224 walikufa huku takriban 4,500 wakijeruhiwa. Kati ya waliokufa, 12 walikuwa raia wa Marekani.

Kufuatia mashambulizi hayo, taarifa ziliibuka kwamba yalikuwa yametekelezwa na watu waliokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kundi la kigaidi la Alqaeda, lililoongozwa na Osama Bin Laden, na ambalo lilikuwa limeapa kuwashambulia Wamarekani kila lilipopata nafasi hiyo.

Ilikuwa ni mara ya kwanza, kwa mujibu wa rekodi zilizopo, kwa kundi la Al Qaeda kutekeleza shambulizi kubwa jinsi hiyo, na ndipo Osama bin laden na wanamgambo wa kundi lake, walianza kupata umaarufu kwani vyombo vya Habari kote duniani vilianza kuwaangazia kwa kina.

Hadi leo, watu 20 wamefunguliwa mashtaka kuhusiana na mashambulizi hayo, na baadhi yao wameuawa, ikiwa ni pamoja na Osama Bin Laden, aliyeuawa na Marekani mnamo May 2, 2011.

Sita tayari wamehukumiwa na wanatumika kifungo cha maisha nchini Marekani hook wachache wengine wakisubiri kesi zao kusikilizwa.

Kwa wakenya na Watanzania, haikuwa rahisi kuelewa ni kwa nini nchi zao zililengwa. Rais wa Kenya wakati huo, ambaye sasa ni marehemu, Daniel Arap Moi, alitembelea eneo la tukio na kuzungumza na shirika la Habari la AP.

"Kwa nini wailenge Kenya? Mnadhani Wakenya wanaweza kuunga mkono jamba kama hili?" aliuliza.

"Kenya imeishi kwa amani na haina chuki na yeyote. Watu wanatakiwa kutatua mizozo yao bila kuwashambulia au kuwatia hofu wengine," alisema Moi.

Tangu tarehe 7 mwezi wa nane mwaka wa 1998, waathiriwa wa mkasa huo wamekuwa wakijiuliza maswali mengi.

Pamoja na kushindwa ni kwa nini walilengwa, pia wamekuwa katika mchakato mrefu wa kutafuta haki.

John Ngige, amekuwa akiongoza msukukumo wa kutaka fidia kwa waathiriwa wote wa mkasa huo. Lakini miaka ishirini na miwili baadaye, hali imekuwaje?

"Hatujaona chchote. Mimi naghisi mawakili waliokuja kwetu kutoka Marekani walitudanganya. Hadi wa leo, tunateseka tu na hata watu wengine wamkufa tangu wakati huo," alisema Ngige katika mahojiano kwa njia ya simu.

Nchini Tanzania, msemaji wa ubalozi wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe aliiambia sauti ya Amerika kwamba wanaendelea kusimama na familia za wale walioathiriwa na shambulizi hilo.

"Tunaungana na Watanzania katika maadhimisho haya hata ingawa mwaka huu hatutafika moja kwa moja kwenye eneo la shambulizi hilo," alisema afisa huyo.

Mnamo mwaka wa 2011, mahakama moja hapa Marekani iliiagiza Sudan kulipa kiasi cha dola bilioni 6 kama ridhaa kwa familia za wamarekani waliothirika katika mashambulizi hayo.

Sudan baadaye ilikata rufaa. Lakini mwezi Mei mwaka huu, mahakama ya juu ya Marekani ilikubaliana na mahakama ya chini kwamba ni lazima Sudan ilipe kiasi hicho cha pesa.

Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Asmaa Abdallah, akizungumza na shirika la Habari la AFP, alisema mwezi Juni kwamba wako katika hatua za mwisho za kutekeleza uamuzi huo wa mahakama ya Juu ya Marekani.

Hata hivyo, kinachowakera waathiriwa raia wa Kenya na Tanzania ni kwamba, familia zao haziko kwenye orodha ya watu watakaofaidika na uamuzi huo, kwani kesi yao, ilirejeshwa kwa mahakama ya chini, na hatma yake kufikia leo, miaka 22 baadaye, haijulikani.

XS
SM
MD
LG