Trump atetea haki ya majimbo kuchukua maamuzi kuhusu utoaji mimba

  • VOA News

Rais wa zamani Donald Trump

Jimbo la Florida, hapa Marekani, limepitisha sheria mpya inayopiga marufuku utoaji mimba, baada ya wiki sita za ujauzito.

Katika kampeni ya urais mwaka huu, muwaniaji Donald Trump, anatetea haki ya majimbo, kuchukua maamuzi kuhusu suala hilo.

Kwa upande wake Rais Joe Biden, anasema hatua kama hiyo, inatishia maisha ya wanawake.

Kampeni ya Biden inafanya haki ya uzazi kuwa kipaumbele cha harakati zake, za kuchaguliwa tena. Makamu wa Rais Kamala Harris alifanya kampeni katika jimbo la Florida katika siku ambayo sheria mpya ya utoaji mimba ilianza kutekelezwa.

Rais Joe Biden

Kamala Harris, Makamu wa Rais anasema: "Hii ni kupigania uhuru. Uhuru wa kimsingi wa kufanya maamuzi kuhusu mwili wa mtu mwenyewe, na siyo serikali yao kuwaambia wanachotakiwa kufanya."

Sheria mpya ya utoaji mimba ya Florida ni miongoni mwa sheria kali zaidi nchini, na imesababisha shinikizo la suala la haki za utoaji mimba kuwekwa kwenye katiba, kupitia uchaguzi wa mwezi Novemba.

Majimbo ya Marekani yanatunga sheria zao kuhusu mimba kwa sababu uamuzi wa Mahakama ya Juu wa 2022, ulikomesha udhibiti wa seriakli kuu kuhusu suala hilo.

Trump aliteua majaji watatu kati ya sita walioamua kesi hiyo, na Harris anasema wapiga kura wanahitaji kumuwajibisha.

Makamu wa Rais Kamala Harris

Kamala Harris, Makamu wa Rais anasema:"Katika taifa letu, tunashuhudia mashambulizi dhidi ya haki za uzazi, kutoka jimbo hadi jimbo. Na elewa ni nani wa kulaumiwa. Rais wa zamani Donald Trump aliyefanya hivyo."

Ingawa Trump anasema sheria mpya ya Florida inavuka mpaka, mara kwa mara anapokea sifa kuhusu uamuzi wa mahakama ya juu, ulioyapatia majimbo uhuru wa kuamua “Ni mapenzi ya watu" alielezea kwenye video kwenye kupitia mtandao wake wa kijamii mwezi uliopita.

Mmiliki wa kliniki Candace Dye anasema kulikuwa na msongamano wa wagonjwa kabla ya sheria mpya ya utoaji mimba. Kwake, marufuku ya wiki sita ni adhabu kali zaidi.

Candace Dye, Mmiliki wa Kliniki anasema: “Wasichana wengi hata hawajui kuwa wana mimba hadi watimize wiki sita. Unajua, wanadhani ni wiki nne, kwa sababu bado hawajaona hedhi. Kwa hiyo, na kisha tunafanya ultrasound yetu."

Nje ya kliniki, waandamanaji wanaopinga utoaji mimba hujaribu kuwasilian na kila mwanamke anayeingia. Tammy Holly anatoa maoni yake.

Tammy Holly, Mwandamanaji wa Kupinga Utoaji Mimba anasema: “Nipo hapa kwa sababu utoaji mimba umeniumiza, na hakika sitaki kuona wanawake wengine wakiumizwa na utoaji mimba. Wanaingia, na wanapotoka wanakuwa tofauti. Hata wajaribuje kuendelea na maisha kama kawaida, hawatafanana kamwe.”

Wakati kukomesha utoaji mimba kukiwapa motisha wapiga kura wengi wa Republican, Trump anaonekana kulichukulia suiala hilo kwa uangalifu wa kisiasa katika kinyang'anyiro cha urais chenye ushindani mkubwa.

Donald Trump, Mgombea Urais wa Republican anaeleza: "Siku zote ongozwa na roho yako, lakini lazima tushinde. Tunapaswa kushinda. Sisi ni taifa linaloshindwa, lakini tunaweza kuwa taifa lisiloshindwa tena. Tutalifanya taifa letu kuwa kuu.”

Harris anasema washirika wa Trump wa chama cha Republican katika Bunge wanataka marufuku ya utoaji mimba itekelezwe nchini kote.

Trump amesema hilo si jambo la lazima kwa sasa, kwamba majimbo yanaweza kujitengenezea sheria za utoaji mimba.