Mbowe na Matiko wanyimwa dhamana, wapelekwa rumande

Freeman Mbowe

Washtakiwa hao pamoja na wengine wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama na kuhamasisha hisia za chuki

Mwenyekiti wa chama cha upinzani huko Tanzania-CHADEMA, Freeman Mbowe pamoja na mbunge wa CHADEMA Tarime Mjini, Esther Matiko wanashikiliwa katika gereza la Segerea baada ya kufutiwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya jijini Dar Es Salaam huko Tanzania.

Kulingana na mahakama viongozi hao wa upinzani walikiuka masharti ya dhamana katika kesi yao ya uchochezi baada ya kusafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri aliyesema kwa kutoka nje ya nchi bila idhini ya mahakama washtakiwa hao walidharau amri za mahakama kwa makusudi.

Kuhusu Mbowe, Hakimu Mashauri alisema kuna mkanganyiko kuhusu taarifa za kuumwa kwake kwani mdhamini wake alieleza kuwa November 8 mwaka 2018 aliugua ghafla na kupelekwa nje ya nchi akiwa mahututi huku wakili wake akieleza kuwa alipelekwa nchini Afrika kusini kwa matibabu.

Kwa upande wa Matiko, Hakimu Mashauri alisema sababu alizozitoa mdhamini wake kwamba alihudhuria ziara ya masuala ya bunge nchini Burundi sio za msingi kwani nchi inaongozwa kwa sheria na kwamba sheria inamtaka mshtakiwa yeyote pamoja na cheo chake alichonacho bado yupo sawa na watu wengine wanyonge.

Kutokana na hatua hiyo Hakimu Mashauri alisema anawafutia dhamana washtakiwa hao wawili na walipelekwa gereza la Segerea ambapo watakaa huko hadi hapo rufaa yao itakaposikilizwa. Kesi imeahirishwa hadi Disemba 6 mwaka 2018.

Hata hivyo baada ya uamuzi huo wakili wa utetezi Peter Kibatala alisema watakata rufaa juu ya uamuzi huo katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kesi hiyo inawahusisha pia washtakiwa wengine wa CHADEMA ambao ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16 mwaka 2018 huko Dar es Salaam.