Ripoti mpya ya Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm (Sipri) kwa mwaka 2018 inaonyesha kuwa katika eneo hilo la Afrika Mashariki, Kenya iliongoza katika manunuzi hayo, kwa kuagiza ndege sita za kivita. Nairobi inategemea kupokea ndege hizo mwaka 2019..
Gazeti la The East African limeripoti Jumapili juu ya utafiti huu. Kenya pia imepokea helikopta nyepesi 8 zilizotumika aina ya Airbus AS-550C3 ikiwa ni msaada kutoka Marekani mwaka 2018.
Ndege sita zilizoagizwa ni pamoja na ndege tatu za usafirishaji aina ya C-271 Spartan kutoka kampuni ya Italian firm Leonardo, ambazo zitagharimu dola za Marekani milioni 200.
Ndege hizi zinakusudia kuchukuwa nafasi ya ndege zilizochakaa aina ya De Havilland Canada DHC-5 Buffalos ambazo zinatumiwa na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).
Ndege nyingine tatu za mizigo mepesi na abiria ni aina ya M28 Skytruck kutoka Poland, zilizokuwa zimeagizwa na Kenya 2016.
KDF pia ilipokea vifaru 12 aina ya Bastion Armoured Personnel Carriers (APCs) vya kubebea silaha na wanajeshi zilizotolewa na Marekani ikiwa ni msaada wa kusaidia kuimarisha ulinzi katika mipaka ya Kenya na kuendeleza ulinzi wa amani Somalia, ambako vikosi vyake vimekuwa vikishiriki katika ulinzi wa amani chini ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika (Amisom).
Kenya ilinunua hizo APCs 12 aina ya MD5 zenye ingine za dizeli kutoka Ufaransa, imeeleza ripoti ya Sipri.
Nchini Uganda, Jeshi la nchi hiyo (UPDF) mwaka 2019 litapokea vifaru aina ya Mamba APCs vinavyotengenezwa Afrika Kusini, na kuunganishwa katika kiwanda cha kutengeneza na kuunganisha magari ya kijeshi kilichoko Jinja, ambacho Rais Yoweri Museveni alikifungua Agosti 2018.
Mwaka 2018, UPDF ilipokea boti 4 za doria za kijeshi aina ya 850 Military Patrol Boats kutoka kampuni ya Twiga Services and Logistics kupitia mkataba wa kampuni ya Impala Services and Logistics, wakati ikiendelea kuboresha vifaa vyake vya doria vya majini.
Ripoti ya Sipri inaonyesha kuwa Uganda iliagiza ndege moja nyepesi ya ujasusi aina ya DA42, modeli ambayo mwaka 2016, ilifanya nchi hiyo kuangazwa na Umoja wa Mataifa baada ya waangalizi wa silaha kuituhumu Kampala kuwa imetumiwa na Sudan Kusini kuinunulia ndege hiyo, wakati vikwazo vya silaha vikiwa vimewekwa dhidi ya Juba.
Nchi nyingine za Kiafrika ambazo zina aina hiyo ya ndege DA42, ambayo aghlabu hutumika kwa ujasusi au mafunzo kwa marubani, ni Nigeria, Ghana, Sudan Kusini na Niger.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania mwaka 2018 ilipokea helikopta tatu aina ya Airbus AS-350 katika manunuzi ya ndege hizo 10 ambazo iliagiza mwaka 2017.
Dar ilikuwa imeagiza helikopta nyepesi nane aina ya AS AS-350/AS-550 Fennec na mbili za usafirishaji aina ya AS-532 Cougar/AS-332 kutoka Romania.
Nchini Rwanda, jeshi la nchi hiyo mwaka 2018 lilinunua makombora ya kuangamiza vifaru 9 aina ya Red Arrow, iliyokuwa imeagiza kutoka China mwaka 2016. Makombora haya yalikuja pamoja na silaha zenye kujifyatua zenyewe tatu aina ya CS/SH-1 122mm, zilizokuwa zimeagizwa mwaka 2017.
Jeshi hilo lilizindua makombora hayo katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi huko kituo cha mafunzo ya kivita cha Gabiro, Disemba mwaka 2018.
Pamoja na nchi hizi kuboresha majeshi yao, kumedhihirika kuwa matumizi yao ya ujumla katika manunuzi ya silaha yameshuka, ikielekezwa kwa Sudan Kusini ambayo imepunguza manunuzi ya silaha kwa zaidi ya asilimia 50 mwaka 2017.
Katika mwaka huo, nchi zote hizi zilitumia dola za Marekani bilioni 2.73 kwa matumizi ya kijeshi, kutoka dola bilioni 2.78 mwaka 2016 na kiwango cha juu cha dola bilioni 3.6 mwaka 2015, kwa mujibu wa takwimu za Sipri.
Kenya iliendelea kuwa yenye matumizi ya juu katika manunuzi ya kijeshi, ikitumia dola milioni 963.5 mwaka 2017, ikifuatiwa na Tanzania iliyotumia dola milioni 593.1, na kisha Uganda iliyotumia dola milioni 444.6 na Rwanda dola milioni 111.
Burundi ilitumia dola milioni 63.9, wakati Sudan Kusini ilitumia dola milioni 72, ikiwa ni punguzo kubwa ukilinganisha na manunuzi ya dola bilioni 1.1 mwaka 2014.
Sipri inatarajiwa kutoa matumizi ya kijeshi ya mwaka 2018 mwezi Mei.