Saa 8.45 asubuhi mapigano yalizuka kama kilometa 31 kutoka Afmadow, mahali ambako majeshi ya Kenya yameweka kambi yao.
Msemaji wa KDF Joseph Owouth amesema idadi isiyojulikana ya magaidi walinusurika huku wakiwa wamejeruhiwa.
Wanajeshi wa KDF ambao wanaendesha operesheni zao chini ya Jeshi la Muungano wa Afrika (Amison) walipambana na magaidi hao.
Kanali Owouth ameongeza kuwa magari ya mizigo iliyokuwa imesheheni silaha nzito na silaha ndogo ndogo zinazomilikiwa na al-Shabaab pia ziliangamizwa.
“Askari wa KDF wamekuwa macho katika ulinzi wao na wataendelea bila ya kusita kuwafuatilia magaidi kuhakikisha kuna amani na usalama nchini Kenya na kuendelea kuzisaidia operesheni za Amisom kwa ajili ya kuiimarisha Somalia,” amesema.
Wakati huo huo Polisi wa Kenya wamesema watu wenye silaha wameteka walimu watatu katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab mashariki mwa nchi hiyo ambako kuna wakimbizi zaidi ya 200,000 wa kisomali.
Ripoti iliotolewa na shirika la AFP leo imeeleza watu watatu waliokuwa na bastola waliteka nyara walimu watatu wa shule ya Udha katika eneo la Hagadera la kambi ya Dadaab.