Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika aeleza sababu za Spika Ndugai kumshinikiza akatishe kikao

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele, ameeleza Jumamosi msimamo wake juu ya kashfa inayomkabili Rais wa Bunge la Afrika, Roger Dang, huku akiwashukuru Watanzania na waafrika wanaomuunga mkono.

Mbunge huyo ambaye ni Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), alikuwa ameshiriki katika uchunguzi wa tuhuma za rushwa ya ngono dhidi ya Rais wa Bunge hilo raia wa Cameroon.

Madai ya Spika Ndugai

Alhamisi, Spika Ndugai, alitangaza bungeni kusitisha uwakilishi wa Mbunge Masele (CCM) katika Bunge la Afrika (PAP) kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema Masele amesema: “Rais anatakiwa apishe ili uchunguzi uweze kufanyika. Ni uchunguzi ambao umekuja na ushahidi ambao umethibitisha kwamba amefanya hivyo na yeye mwenyewe amekiri amefanya, ameomba msamaha, lakini haitoshi lazima uchunguzi zaidi ufanyike ili kukomesha tabia hii.”

“Wewe Rais wa Bunge unatumia mamlaka yako vibaya kumwandikia Spika wa Bunge la Tanzania kwamba nirudi nyumbani, mimi sirudi kwasababu sikuchaguliwa na wewe, hawa waheshimiwa wabunge ndio walinichagua na ndio wenye mamlaka ya kuniondoa,” Mbunge huyo alisisitiza.

Masele kuendelea kusimamia haki

Masele kwenye ukurasa wake wa Twitter Ijumaa aliandika ataendelea kusimamia haki, ukweli na uadilifu bila woga hadi kieleweke.

“Nawashukuru wote kwa kuniunga mkono nitasimamia haki, mimi ni baba wa mtoto mmoja wa kike siwezi kuvumilia hali hii nawaomba wenzangu wote tupige kelele kuhusu unyanyasaji wa kingono kuanzia shuleni, sehemu za kazi na kwenye jamii tunazoishi na duniani kote,” alisema Masele.

Masele alipongeza ushujaa wa wote ambao walijitolea kutoa maelezo kuhusu unyanyasaji uliyokuwa unafanywa na Rais huyo wa Bunge la Afrika na kuwataka wengine kuiga mfano huo.

Ujumbe wa Video

Kupitia ujumbe wa video fupi iliyosambaa mitandaoni wakati Masele akihojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili Rais wa PAP, alisema amefurahi baada ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa na Bunge hilo kuchunguza tuhuma hizo zinazomkabili Rais kukamilisha kazi yake.

“Mimi kama mkuu wa utawala na wafanyakazi wote nina wajibu wa kuhakikisha kwamba hali za wafanyakazi hususan wanawake ambao wanamtuhumu Rais kuwanyanyasa kijinsia, kingono, utafiti unaonyesha kwamba Rais anakesi ya kujibu hivyo tutaikabidhi Umoja wa Afrika kwa ajili ya uchunguzi wa kina,” alisema.

Serikali ya awamu ya nne

Masele, katika serikali ya awamu ya nne, alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na baadaye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), kwa sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa PAP.

Kutokana na uamuzi huo wa Spika Ndugai, Masele ambaye kwa sasa yuko nchini Afrika Kusini kwenye vikao vya PAP, ametakiwa kurejea nchini ili kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku akidokeza kuwa hata Kamati ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nayo itamhoji.

Tuhuma zaidi za Spika Ndugai

Ndugai alisema katika uwakilishi wa Masele kwenye Bunge hilo la Afrika, kumejitokeza matatizo makubwa ya kinidhamu.

“Nisingependa kuyafafanua leo (juzi) muda hautoshi. Tumelazimika kumtafuta Masele kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu, badala yake amekuwa akionyesha kugoma. Hata jana (Jumatano) kwenye Bunge hilo tumeona 'clips' zilionyesha akihutubia Bunge hilo japo ameitwa na Spika.

"Baada ya kumwandikia arudi nyumbani, aje ahudhurie kwenye Kamati ya Maadili, akahutubia Bunge akisema japo ameitwa na Spika, ameambiwa na Waziri Mkuu akaidi wito wa Spika, aendelee na mambo yake kule, kitu ambacho ni uongo na kuidhalilisha nchi," alisema.

Kiongozi huyo wa Bunge la Tanzania alidai Masele ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya ovyo ovyo ndiyo maana ameitwa kwenye Kamati ya Maadili.

"Tumemwita aje atufafanulie, huenda yuko sahihi, lakini kwa mtazamo wetu, tunaona anafanya mambo ya hatari ikiwamo kugonganisha mihimili," Ndugai alisema.

"Amekuwa akipeleka mhimili wa juu kabisa wa serikali maneno mengi ya uongo na kudhalilisha Bunge na ushahidi upo. Ni kiongozi ambaye amejisahau, sijui anatafuta kitu gani. "Hizo vurugu ambazo anazionyesha kwenye Bunge lake huko, sisi hazituhusu sana. Tumemwita aje kwa mambo ya hapa nyumbani ya utovu wa nidhamu.

Spika amwandikia Rais wa PAP

"Kwa kuwa tumekuwa tukimwita hapa nyumbani tangu Jumatatu hataki kurudi, nimemwandikia barua Rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi wa Stephen Masele katika Bunge la PAP hadi hapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itakapokamilisha uchunguzi na tuhuma dhidi yake."

Kwa upande wake Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), amehoji nafasi ya wabunge wanaochaguliwa na Bunge kuliwakilisha katika mabunge mengine duniani, kusimamishwa na Kiti cha Spika bila uamuzi huo kujadiliwa na waliowachagua.

Baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali' bungeni jijini Dodoma, Ijumaa, mbunge huyo alisimama na kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliyekuwa anaongoza kikao, akihoji uhalali wa Kiti cha Spika kuwasimamishwa wawakilishi waliochaguliwa na chombo hicho cha kutunga sheria.

Mbunge Msigwa ahoji

"Uhalali unatoka wapi na hawa hawakuteuliwa, wamechaguliwa? Na nilitaka kujua anasimamishwa na kiti bila kujadiliwa, inatuchafua kama taifa. Bunge litakuwa na nguvu gani ya kuwalinda hawa tunaowachagua?" Msigwa alihoji.

Mbunge huyo alisema ameona ahoji kuhusu suala hilo baada ya juzi Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutangaza kusimamisha uwakilishi wa Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele (CCM) katika Bunge la Afrika (PAP) akimtuhumu kwa utovu wa nidhamu.

Akimjibu Msigwa, Mwenyekiti wa Bunge, Chenge, alimtaka mbunge huyo kutowahisha hoja kwa kueleza kuwa tayari Spika Ndugai amelitolea uamuzi suala hilo.

Kauli ya Chenge

Chenge ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliwataka wabunge kusubiri hadi taarifa ya suala hilo itakapowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na watakuwa na nafasi ya kujadili.Alisema kwa sasa milango bado haijafungwa kwao kulijadili suala hilo, lakini ni lazima taratibu za uendeshaji wa shughuli za Bunge zifuatwe.

Katika taarifa yake ya juzi bungeni, Spika Ndugai alimtaka Masele ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa PAP, kurejea nchini kutoka Afrika Kusini anakohudhuria vikao vya PAP, ili kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Kiongozi huyo wa Bunge la Tanzania pia alieleza kuwa baada ya kumalizana na kamati ya Bunge, Masele pia atahojiwa na Kamati ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu.