Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 15:11

Bunge la Tanzania latoa ufafanuzi juu ya kutotambuliwa CUF-Maalim Seif


Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Job Ndugai
Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Job Ndugai

Bunge la Tanzania limetoa ufafanuzi juu ya sababu zilizopelekea taasisi hiyo kutomtambua Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, amedai kuwa Maalim Seif hatambuliwi na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Amesema pia licha ya kiongozi huyo, pia hawezi kufanya kazi na wabunge waliofukuzwa na chama hicho kwani utaratibu ulifuatwa na sasa ofisi yake inajiandaa kuwaapisha wabunge wapya Septemba 5, bungeni mjini Dodoma.

Hivi karibuni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alilalamikiwa na chama cha upinzani CUF nchini Tanzania kutokana na kile wanachodai kuwa ni hujuma anazozifanya dhidi ya chama hicho.

Mutungi ameshutumiwa na Katibu Mkuu wa CUF kuwa amekuwa akishirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba kukihujumu chama hicho.

Maalim Seif alieleza hayo Ijumaa (Agosti 19) katika barua yake ya kumjibu Jaji Mutungi kuhusu hatua yake ya kuwatambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF na Magdalena Sakaya kama kaimu katibu mkuu pamoja na kuwa watu hao tayari walishasimamishwa uanachama kwa tuhuma mbalimbali.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania Katibu mkuu huyo alifikia uamuzi wa kumjibu Jaji Mutungi baada ya ombi lake la kuwafukuza uanachama wabunge wawili; Sakaya (Kaliua) na Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) kugonga ukuta.

Madai ya CUF ni kuwa Profesa Lipumba alimweleza Msajili kuwa Maalim Seif ameshindwa kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutofika ofisi ya chama hicho zilizopo Buguruni, hivyo akamteua Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Bara kukaimu ukatibu mkuu.

“Kwa mujibu wa katiba ya CUF mimi, Maalim Seif bado ni katibu mkuu wa chama hiki na nipo hapa nchini, ni mzima na nina akili timamu. Na nafasi yangu haiwezi kukaimiwa na Sakaya ambaye tulishamsimamisha uanachama,” ilieleza barua hiyo.

Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema Spika Ndugai ameeleza msimamo huo ni suala la utaratibu kwa sababu mwenye kumbukumbu za vyama vya siasa na viongozi wake halali ni Msajili wa Vyama vya Siasa.

Alisema ikiwa atasema kuwa hamfahamu mtu na yeye lazima asimfahamu kwani ndiyo utaratibu wa kazi unavyotaka.

“Sasa siwezi kuzuka nikawa nawatambua watu ambao hawatambuliwi na BRELA, kwa maana hiyo ya makampuni na kadhalika na msingi huo siwezi kuwatambua watu ambao hawatambuliwi na msajili,” alisema Spika huyo.

“Kwa sababu huko ndiko vyama vinakopeleke Katiba zao, huko ndiko vyama vinakopeleka mabadiko ya kumbukumbu zao za mikutano ya mabadiliko yoyote yale,” alisema Ndugai.

Aliendelea kufafanua kwamba tangu Machi mwaka huu, alipata barua kutoka kwa Msajili iliyomweleza kwamba amepata taarifa rasmi kuwa Maalim Seif hayupo ofisini, kwa msingi huo majukumu ya chama hicho yatatekelezwa na Naibu Katibu Mkuu wake hadi hapo itakapoelezwa vinginevyo.

“Kwa hiyo huo ndio msimamo wa tangu Machi kwa mujibu wa barua niliyokuwa nimeandikiwa kama rekodi ya kufanyiwa kazi, sasa ninapoletewa barua na mtu huyo baadaye ungekuwa wewe ungefanyaje wakati umekwisha arifiwa kwamba huyo mtu hayupo ofisini? Sasa swali la kwanza ni kumuuliza huyo mtu amekwisha rudi ofisini? Akikwambia hapana, sasa barua naandikia wapi, (wilaya ya )Kongwa?

“Kwa hiyo inakuwa ngumu kidogo. Ni tatizo la kwao, hamuwezi kumlaumu Spika au mtu mwingine. Ni usafi wa kufanya ndani kwao wenyewe, wakifanya usafi wao sisi wala hatuna tatizo. CUF ikisema inakutambua wewe sisi tutapinga? Hili ni la kwao na wanajua zaidi wao kuliko sisi, tuwaachie wao wenyewe wenye jukumu la kusafisha nyumba yao,” alisema Ndugai.

XS
SM
MD
LG