Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 11:40

Wadau Tanzania waituhumu serikali kwa kukandamiza uhuru wa habari


Dkt Abbas
Dkt Abbas

SERIKALI ya Tanzania imetaka magazeti, majarida na machapisho mbalimbali kuomba upya leseni za kuendesha shughuli zake, jambo ambalo kwa sasa litakuwa likifanyika kila mwaka.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa habari wamekosoa hatua hiyo, wakisema inaonyesha dhana ya ukandamizaji wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.

Kutokana na taarifa hiyo ya serikali, wadau mbalimbali walitoa maoni yao, huku wakikosoa kilichotangazwa na Serikali, vyanzo vya habari nchini Tanzania vimeripoti Alhamisi.

Mwanahabari mkongwe ambaye pia ni mwanasheria, Jenerali Ulimwengu, amesema: “Tangazo la leo (jana) ni kuendeleza sheria mbovu ambayo ni kandamizi na kumaliza kabisa uhuru wa habari na mawasiliano.

“Tulipinga mahakamani… hata wale walioona sheria hii ni nzuri watakuja kuona ni mbaya, uhuru wa habari katika nchi hii haupo tena.

“Tujiandae kuwa na jamii ambayo haitakuwa na vyombo vya habari, isipokuwa vipaza sauti vya Serikali na chama tawala,” alisema Ulimwengu wakati akihojiwa na gazeti la Mtanzania.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alisema sheria hiyo ilipitishwa hivyo hakuna namna, pamoja na kwamba ina makandokando mengi, wanalazimika kuitekeleza.

Alisema kitendo cha kusajili gazeti kwa Sh milioni moja kila mwaka ni maumivu na kwamba kuna uwezekano baadhi ya magazeti yakafa kwa sababu ya gharama hiyo.

Balile aliliambia gazeti la Mtanzaniakwa sasa gazeti moja litakuwa na leseni mbili, moja ya jiji au halmashauri na hiyo mpya iliyotangazwa jana.

“Hapa hawakutoa maelezo ya kutosha kwamba leo unasema lisajili upya sasa ukipata hiyo leseni ya Maelezo ile ya jiji inafutika? Inakuwaje biashara moja kuwa na leseni mbili?” alihoji Balile.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakari Karsan, alisema hivi sasa ukandamizaji wa vyombo vya habari umeanza kwa kuwataka watu waseme vile Serikali inavyotaka.

“Ukandamizaji umeanza kwa kutumia ‘system’ (mfumo)… sasa mnasajiliwa ili watu waseme Serikali inavyotaka. Sheria hiyo tumeipinga sana na bado pingamizi liko mahakamani,” alisema Karsan.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema lengo la sheria hiyo ni kuminya uhuru wa habari kwa sababu vyombo hivyo vina vipato kidogo, hivyo ni vigumu kupata Sh milioni moja kila mwaka.

“Kuna vyombo haviko kibiashara, vipo kwa ajili ya kuhabarisha umma, itakuwa ngumu kwao kupata hiyo fedha, hili tulilipinga sana na bado tunapinga,” alisema Bisimba.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, alisema sheria hiyo haikupaswa kufanya kazi peke yake bali ilitakiwa kuwa pamoja na ile ya haki ya kupata taarifa.

“Sheria hii haikupaswa kufanya kazi peke yake bali na ile sheria mama ya haki ya kupata taarifa, lakini kumbe hawa ni danganya toto, wanataka hii ya kudhibiti vyombo vya habari.

“Kuna mambo yanakosekana katika sheria hii, kwanza haki ya waandishi na wananchi kupata na kutafuta taarifa.

“Sheria hii imeanza kufanya kazi kinyume na taratibu na sheria pacha, kama pacha mmoja anapelekwa shule halafu mwenzake anaachwa inakuwa ni ajabu.

“Sheria hii imekuja, sasa imegeuka nyundo ya Serikali kudhibiti vyombo vya habari,” alisema Kibamba.

Novemba 16 mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alitia saini sheria hiyo baada ya kupitishwa na Bunge, huku kukiwa na mvutano mkubwa kati ya wadau wa habari na Serikali kwa upande mmoja na Bunge kwa upande mwingine.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, akizungumza na waandishi wa habari Jumatano Dar es Salaam, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Wamiliki wa magazeti na majarida ambao wana usajili kwa sasa, wanatakiwa kuomba usajili mpya kuanzia Jumatano hadi Oktoba alisema utaratibu huo mpya utawahusu wamiliki wote wa magazeti (Newspaper), majarida (journals, magazines na newsletters).

Dkt Abbasi alisema baada ya muda huo, magazeti na majarida ambayo hayatasajili upya, hayataruhusiwa kuchapishwa kwani yatakuwa yametenda kosa la jinai.

Alisema utoaji huo wa leseni ni kwa matakwa ya kifungu cha 5 (e) cha sheria hiyo na kwa kanuni ya 7 ya kanuni za sheria za habari za mwaka 2017, zilizochapishwa kwenye tangazo la Serikali Na 18 la Februari 3.

Sheria na utaratibu wa sasa unafuta mfumo wa awali wa utoaji wa hati za usajili wa magazeti na majarida, uliokuwa ukitumika kwa mujibu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo kwa sasa imefutwa.

“Aidha leseni hizi zitahuishwa kila mwaka kwa mujibu wa kanuni za 8(3) na 12(1)(2) za kanuni za sheria ya huduma za habari mwaka 2017,” alisema Dkt Abbasi.

Akizungumzia taasisi za Serikali, alisema zenyewe kigezo cha cheti cha usajili wa kampuni hakitazihusu, badala yake watatakiwa kuwasilisha barua kutoka kwa mtendaji mkuu wa taasisi.

XS
SM
MD
LG