Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 02:06

Chadema kupinga uamuzi wa Spika Ndugai kumvua Nassari ubunge


Joshua Nassari
Joshua Nassari

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Arusha, nchini Tanzania kimemtaka Mbunge Joshua Nassari, aliyevuliwa ubunge na Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kukusanya vielelezo vyote ili shauri hilo lichukuwe mkondo wa kisheria.

Uamuzi huo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kumvua ubunge Nassari ambaye alikuwa mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), umepokelewa kwa hisia tofauti. Baadhi ya wananchi wa Jimbo lake wamesema kuwa uamuzi huo ni muwafaka.

Mbowe ataka busara itumike

Lakini Mwenyekiti wa Chadema wa Taifa Freeman Mbowe wiki iliyopita alisema kitendo hicho cha kumvua ubunge Nassari siyo cha kibinadamu, hasa ikizingatiwa kuwa Mbunge aliyevuliwa ubunge alikuwa amefuata taratibu za kuijulisha ofisi ya Spika kuhusu udhuru wake wa kutokuwepo bungeni, na ametaka busara itumike katika uamuzi huo.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Arusha Aman Golugwa, ameliambia gazeti la Mtanzania kuwa watapeleka vielelezo hivyo ili vyombo vya sheria vitafsiri uamuzi uliofanywa na Spika Ndugai.

"Chama kipo na Nassari imara kuhakikisha tunachukua hatua za haki. Ndio maana tumemwambia akusanye vielelezo vyote vya taarifa alizoandika kwetu na kwa Spika,” alisema Golugwa na kuongeza:

Nassari alikuwa anahudhuria matibabu ya mkewe

“Sisi hatuoni utoro hapo wa kutohudhuria vikao vya Bunge kama taarifa inavyojieleza, kwani alikuwa anatoa taarifa za kuhudhuria masomo nje ya nchi pamoja na matibabu ya mke wake.

“Kwenye mikono ya sheria tunaamini hakuna wanasheria wala majaji watakaovumilia jambo hili.

“Lakini alikuwa akihudhuria vikao vya Kamati za Bunge, uthibitisho upo posho alizokuwa analipwa kwenye vikao vya Kamati ushahidi upo, pengine kesho Nassari atazungumza na wanahabari,” alisema.

“Hapa hatutetei ubunge tu, tunaangalia kwa upana mzima kwamba unawaondolea wananchi mwakilishi wao kwa utaratibu gani, ili tu uchaguzi uitishwe tena kwa mamilioni ya fedha,” alisema Golugwa.

Madai ya Spika juu ya Nassari

Nassari alivuliwa ubunge juzi kutokana na madai ya Spika kuwa hakuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo, huku mwenyewe akisema amepokea taarifa hiyo akiwa kwenye kazi za kibunge mkoani Kilimanjaro na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Kuvuliwa ubunge wa Nassari kunafanya Chadema kupoteza wabunge nane tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015, ambapo kati yao saba walijiuzulu uanachama wa chama hicho na baadaye kuteuliwa tena kuwania nafasi zao kupitia CCM.

Juzi Spika wa Bunge, Ndugai, alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, kumtaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi.

Taarifa hiyo ilieleza sababu za Nassari kuvuliwa ubunge kuwa ni kutohudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo. Pia ilitaja mikutano hiyo kuwa ni mkutano wa 12 wa Septemba 4 hadi 14, 2018, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16, 2018 na ule wa 14 wa Januari 29 hadi Februari 9, mwaka 2019.

Uamuzi umefuata katiba

Taarifa hiyo ilisema: “Uamuzi huo wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 71(1) (c). Ibara hiyo inaeleza kuwa ‘Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

"Ibara hiyo pia imefafanuliwa katika kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, kuwa ‘kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge, mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi."

Taarifa hiyo ilisema: “Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Arumeru Mashariki.”

XS
SM
MD
LG