Zitto alitoa kauli hiyo Jumamosi baada ya mahojiano na gazeti la Mtanzania kutaka ufafanuzi wa baada ya Ndugai kukaririwa na Kituo cha Televisheni cha Azam akisema kwamba hata kama hakuna kanuni iliyoandikwa, lakini akiwa kama kiongozi wa Bunge anao uwezo wa kumnyamazisha Zitto kwa muda wote bungeni.
Katika maelezo yake kwa gazeti la Mtanzania, Zitto, alisema hana maoni mengine dhidi ya kauli ya Ndugai kwa sababu ameishapelekwa katika Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Malumbano kati ya Ndugai na Zitto yalianza mapema wiki hii baada ya kiongozi huyo wa ACT–Wazalendo kudai kuwa Bunge limewekwa mfukoni na Serikali wakati alipotoa maoni kuhusu ripoti mbili za Kamati ya Bunge kuhusu biashara ya madini ya almasi na tanzanite.
Kufuatia kauli hizo, Ndugai, aliagiza Zitto ahojiwe na Kamati ya Maadili huku akimshtaki kwa wapiga kura wake kuwa licha ya mbunge wao kuwapo nchini, lakini hajafika bungeni kuwawakilisha na yeye (Spika) hana taarifa.
Ndugai alisema bungeni kuwa ana uwezo wa kumpiga marufuku Zitto kuzungumza hadi miaka yote mitano iishe na hana pa kwenda, hawezi kuuliza swali lanyongeza wala kuzungumza na hakuna atakachoweza kumfanya.
Lakini Zitto alimjibu kupitia ujumbe alioutuma katika akaunti yake ya Twitter akisema: “Nimegundua Spika Ndugai ameibua mashtaka yangu ili kufunika ufuatiliaji wa wananchi kuhusu (Tundu) Lissu kupigwa risasi. Nimeamua sitawapa hilo.”
Septemba 27, mwaka huu, Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) alipigwa risasi kati ya 28 hadi 32, mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge na sasa uko Nairobi nchini Kenya akitibiwa.
Katika mahojiano na kituo cha Azam Tv kuhusu tathmini ya kikao cha nane cha Bunge la 11 Jumamosi, Ndugai, aliulizwa na mwandishi kuhusu kanuni zinazompa nafasi ya kumnyamazisha mbunge.
Katika maelezo yake, Ndugai, alisema si kila kitu huandikwa katika masuala ya kikazi kwa sababu kiongozi wa kazi ana mamlaka makubwa na madaraka makubwa kuliko yaliyoandikwa.
“Sio kila jambo lazima iwe kanuni, narudia tena nimesikia watu wakibishabisha, ninao uwezo, ninao uwezo, ninao uwezo kama Spika. Ukisoma kanuni za Bunge kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho ni Spika, Spika, Spika na zipo kanuni ambazo zinamruhusu Spika kwa kadiri anavyoona inafaa, kwa busara yake namna gani aongoze Bunge.
“Huwezi kuwa unatukana Bunge, unamtukana huyo Spika halafu huyo huyo anakupa nafasi uzungumze, kwani yeye ni malaika? Mimi ni binadamu wa nyama kama binadamu mwingine. Kwa kadiri ambavyo unaninyanyasa na kunidhalilisha mbele ya watu na mimi nitatumia madaraka yangu na mamlaka niliyonayo ambayo nimepewa na nchi na nimepewa na Mungu kuona nini nifanye katika mamlaka niliyonayo,” alisema.