Kesi ya Tundu Lissu : Uamuzi wa Mahakama Kuu wasubiriwa juu ya kuapishwa Mbunge - mteule wa CCM

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai

Uamuzi wa Mahakama Kuu juu ya hatma ya kuapishwa kwa mbunge mteule wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unasubiriwa kwa shauku kubwa ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mujibu wa mawakili wa Tundu Lissu uamuzi huo unatarajiwa kutolewa Jumatatu na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iwapo itatoa zuio la kuapishwa kwa mbunge huyo wa CCM au la.

Katika maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na kaka wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu, Alute Mungwai Lissu, pamoja na mambo mengine, ameiomba Mahakama hiyo itoe zuio la kuapishwa kwa mbunge huyo mpya na ruhusa ya kumshtaki Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa kumvua ubunge pasipo sababu za msingi.

Gazeti la Nipashe limeripoti hapo awali Mahakama hiyo ilitupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na upande wa Jamhuri uliotaka kesi hiyo isisikilizwe mahakamani hapo, kutokana na walichodai ni mapungufu ya kisheria ya maombi hayo, hivyo kutaka yasisikilizwe.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu, Sirilius Matupa, aliyatupa mapingamizi hayo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili kwa maelezo kwamba upande wa Jamhuri haukuwa na hoja za msingi za kuizuia kesi hiyo isisikilizwe mahakamani hapo, na hivyo kukubaliana na hoja za Wakili wa Lissu, Peter Kibatala.

Katika maombi namba 18 ya mwaka 2019, Tundu Lissu ameiomba Mahakama impe kibali cha kufungua kesi dhidi ya Spika Ndugai na ili mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika ampe taarifa ya kumvua ubunge.

Hati ya dharura aliyowasilisha Lissu inaiomba mahakama isikilize na kutoa uamuzi haraka kabla ya kuapishwa kwa mbunge mteule Mtaturu, ambaye ndiye hivi sasa mrithi wai kiti hicho, baada ya kutangazwa mshindi kwa kupita bila kupingwa.

Mnamo Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Ndugai alitangaza uamuzi wa kumvua ubunge Tundu Lissu kwa maelezo kuwa alishindwa kuhudhuria vikao kwa muda mrefu bila kumjulisha pamoja na kutokujaza taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.