Wakenya waeleza dukuduku lao baada ya shambulizi la abiria Mandera

Jeshi la Polisi nchini Kenya likiweka kizuizi baada ya shambulizi la kigaidi Mandera, Kenya, Ijumaa Aprili 12, 2019.

Wakenya wamekasirishwa na shambulio jingine la kigaidi Jumatano lililouwa abiria wanne katika Kaunti ya Mandera, Kenya.

Pia abiria kadhaa walijeruhiwa wakati basi la Moyale Raha likitokea Mandera kuelekea Nairobi kushambuliwa na watu wasiojulikana waliokuwa na bunduki.

Zawadi Emmanuel Naibei, wa Eldoret, Kenya kupitia mtandao wa kijamii wa voaswahili Facebook analaumu serikali kutoweka ulinzi kwa raia wake, “lakini ule ubinafsi unapoingilia katika uongozi ndipo kila kitu kinakwenda mrama.”

Anaongeza kuwa mashambulizi mengi Kenya yamefanywa na vijana wa humu nchini. Kisa kikiwa ni kukosa ajira inayowalazimu vijana hawa kujiunga na makundi haya haramu ili angalau wapate riziki ya kujikimu kimaisha licha ya kutambua hatari inayowakumba…”

Kapedo Shem wa Naivasha Kenya kupitia mtandao wa voaswahili anasema bado vyombo havijakabiliana na tishio lile la magaidi kwa sababu “tunaona hapa Kenya kila mara wanawaua raia wasiokuwa na hatia.”

Naye Nicholas Wamunyinyi Juma wa Nairobi, Kenya anasema kuwa anaona hakuna juhudi zinazo fanyika kabisa. “Wange weka hali kamilifu kuzuia, sio kukimbilia wakati magaidi wamelipua mahali.”

Michael Kwena wa Marsabit kaskazini mwa Kenya anasema makundi ya kigaidi yamesalia kuwa tishio kubwa kwa usalama hasa hapa Kenya.

“Hata leo, al-Shabaab wamelivamia basi la abiria lililokuwa linatoka mandera kuelekea Nairobi ambapo inahofiwa kuwa, watu watatu walipigwa risasi na kuuwawa. Juhudi zaidi zinahitajika na pia maafisa wa kijasusi wanastahili kuongezwa katika maeneo yanayotazamiwa kama hatari…”

Benard Kirui kutoka Londiani Kericho Kenya anaeleza vyombo vya usalama abadani hawatekelezi majukumu yao, maafisa wakuu wa ulinzi wamejiingiza katika siasa wakiangazia macho vitu vya kisiasa, siwatambui Mimi, mashambulizi ya kigaidi yaliyo shuhudiwa Jumatano huko Moyale ndio dhihirisho tosha.

Reuben Alutsachi wa Kakamega Kenya anasema : “Maoni yangu ni Serikali haijafanya vya kutosha kukabiliana na ukaidi.

Lakini Jospato Kabitungu anafikiri kuwa vyombo vya usalama viko imara Kenya, “serikali yetu imeweza kudhibiti mashambulizi ya al-Shabaab kabisa kwa kushirikiana na Wakenya na hata nchi nyingine .

Mashuhuda wa shambulizi hilo wameeleza kuwa watu hao wenye bunduki walijaribu kulizuia basi lakini dereva aliendesha basi hilo kwa kasi na wakaanza kurusha risasi na kupiga magurudumu na kulizuia basi.

Walioshuhudia tukio hilo wamesema baadhi ya abiria walifanikiwa kukimbia.

Akihojiwa na Sauti ya Amerika Kamishna wa Kaunti ya Mandera Onesmus Kyatha amesema uchunguzi unafanywa kwa wakati huu na kwamba abiria wengi walinusurika kwa vile polisi waliokuwa karibu walifika kwa haraka.

Wanamgambo wanaodhaniwa ni wa kundi la al-Shabaab wanalaumiwa kwa mashambulio ya mara kwa mara katika eneo hilo la kaskazini mashariki ya Kenya.

Shambulio jingine kama hilo lilitokea mwezi uliyopita katika mji wa Witu, Kaunti ya Lamu, ambapo watu watatu waliuawa Mwezi Disemba 2019.