Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 02:00

Shambulizi katika kambi inayotumiwa na jeshi la Kenya, Marekani ladhibitiwa


Ramani ya Kenya
Ramani ya Kenya

Serikali ya Kenya imesema imefanikiwa kudhibiti shambulizi la kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab Jumapili katika kambi ya kijeshi inayotumiwa na wanajeshi wa Kenya na Marekani, bila ya kuwepo madhara yoyote.

Kundi hilo lilidai limefanya mashambulizi mapema Jumapili, dhidi ya kambi hiyo ya kijeshi nchini Kenya.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Luteni Kanali Paul Njuguma ametoa ufafanuzi kuwa wapiganaji walivamia uwanja wa ndege wa Manda na sio kambi ya jeshi ya Simba, kama ilivyodaiwa hapo awali na Al-Shabaab. Amesema uwanja huo wa kiraia pia unatumika kama lango la kuingilia kambini hapo.

"Hiyo ilikuwa propaganda," alisema Njuguna, akipinga madai ya Al-Shabaab. Katika ujumbe wa Twitter, KDDF ilisema: "Alfajiri ya leo majira ya saa 11:30, kulikuwepo na jaribio la kuvuruga usalama katika uwanja wa ndege wa Manda. Jaribio hilo lilizuwiwa kwa ufanisi."

"Mpaka sasa miili minne ya magaidi imegunduliwa. Uwanja wa ndege uko salama," uliendelea kusema ujumbe huo wa Twitter. Hakujaripotiwa maafa yoyote kwa wanajeshi wa Marekani au Kenya.

Jeshi la Kenya limesema moshi unaoonekana kwenye mkanda wa video kutoka eneo la tukio unatoka kwenye gari la mafuta lililoathiriwa katika shambulizi hilo, na tayari umedhibitiwa "na tayari hatua ya kuimarisha usalama zimechukuliwa."

Kambi ya Simba iliyoko Manda Bay, kaunti ya Lamu nchini Kenya ndio ambayo Al-Shabaab ilidai kuishambulia.

Kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) pia ilituma ujumbe wa Twitter, ikikiri kwamba ilikuwa inafuatilia hali hiyo.

Lakini katika taarifa yake haikutoa maelezo zaidi. Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi kadhaa yanayoilenga Al-Shabaab nchini Somalia.

Marekani inavisaidia vikosi vya Somalia pamoja na wanajeshi wa Umoja wa Afrika (AU) katika kupambana na kundi la Al-Shabaab, ambalo lina mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda.

XS
SM
MD
LG