Jeshi, raia wafikia mwafaka kushirikiana Sudan

Mjumbe wa Umoja wa Afrika Sudan Mohamed al-Hacen Lebatt (kushoto) akiwa na naibu mkuu wa baraza la utawala wa jeshi Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Khartoum, Sudan.

Uongozi wa kijeshi nchini Sudan na muungano wa vyama vinavyotetea demokrasia wamefikia makubaliano ya kugawa madaraka kwenye serikali ya mpito, kabla ya kuunda serekali ya kiraia ilio huru itakayoongozwa na waziri mkuu.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika (AU) Mohammed el Hassan Labat Ijumaa, amewambia waandishi wa habari kwamba pande zote mbili zimeafikiana kuunda uongozi wa awamu mbili ukiwashirikisha wanajeshi na raia, uongozi ambao utadumu kwa miaka mitatu.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo ya siku mbili yaliyofanyika mjini Khartoum ili kumaliza ghasia za wiki kadha tangu jeshi limuondowe madarakani rais wa muda mrefu Omar al Bashir mwezi April 2019.

Mazungumzo juu ya ugavi wa madaraka yalikwama Juni 3 kufuatia jaribio la utawala wa kijeshi kutaka kuzima kimabavu maandamano yaliokuwa yanafanyika mjini Khartoum.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC