Hatma ya madaktari wawili ambao ni raia wa Cuba bado haijulikani baada ya ripoti za kutekwa nyara na magaidi wa al-Shabaab kaskazini mashariki mwa kenya. Inadaiwa kuwa huenda madaktari hao wamevushwa hadi nchini jirani ya Somalia .
Madaktari hao ni miongoni mwa kundi la madaktari zaidi ya 100 kutoka Cuba waliowasili Kenya kwa ombi la serikali kufanya kazi kuziba pengo la uhaba wa madaktari .
Msemaji wa polisi nchini Kenya Charles Owino amethibitisha kuwa mlinzi wa madaktari hao ameuawa na magaidi ambao tayari walitoroka na gari na kuingia Somalia.
Wakati huohuo vyanzo vya habari nchini Kenya vinasema kuwa dereva wa gari la serikali ya jimbo la Mandera ambalo madakatari hao walikuwa wakilitumia limepatikana na dereva wake anahojiwa.
Hii sio mara ya kwanza kwa raia wa kigeni kutekwa nyara, mwaka 2018 raia wa Utaliano Sylvia Constanca Romano alitekwa nyara eneo la pwani ya Kenya na hadi sasa bado hajapatikana.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC.