Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 13:57

Wanaopinga kura ya maoni Misri wadai ni njama za udikteta


Bango linalounga mkono mchakato wa marekebisho ya katiba ya Misri kwa kumuongezea muda wa uongozi Rais Abdel-Fattah el-Sissi, Cairo, Misri, April 16, 2019.
Bango linalounga mkono mchakato wa marekebisho ya katiba ya Misri kwa kumuongezea muda wa uongozi Rais Abdel-Fattah el-Sissi, Cairo, Misri, April 16, 2019.

Wananchi wa Misri wanapiga kura Jumamosi kutoa maoni yao juu ya kufanyika mabadiliko ya katiba yatakayo mruhusu Rais Abdel-Fatah el-Sissi kubakia madarakani hadi mwaka 2030.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa kura hiyo ya maoni imeitishwa wakati wakosoaji wa el -Sissi wakiandamwa na nguvu ya dola.

Serikali ya Misri inaendelea kuwazuilia jela maelfu ya watu, wengi wao wakidaiwa ni wafuasi wa itikadi kali ingawa wachambuzi wanaeleza kuwa kuna wanaharakati wa kawaida pia kati ya hao walioko jela.

Wanaongeza kuwa hali hiyo imesaidia kurejesha nyuma vuguvugu la uhuru uliopatikana mwaka 2011 katika kudai utawala wa kidemokrasia.

Wanaounga mkono kura hiyo ya maoni wamepongeza hatua hiyo kama ni jukumu la kitaifa, lakini wakosoaji wanalaumu kuwa kura ya maoni kwa kifupi ni hatua ya kuhodhi madaraka yote nchini ambako ushiriki wa kisiasa kwa wote umedidimizwa kabisa.

Wanaeleza kuwa upinzani ni kama haupo, wakati viongozi wengi maarufu, wafanyabiashara na vyombo vya habari vimeungana na serikali iliyoko madarakani.

Maafisa wameahidi kutangaza matokeo ya kura hiyo Aprili 27 na kusema iwapo kadhia hiyo itapitishwa, watafanya marekebisho ya katiba mara moja.

Mengi katika hayo marekebisho yanahusiana na muundo wa serikali, kuanzisha nafasi mpya na kuongeza idadi ya wateule wa rais.

Jeshi la Misri, ambalo tayari linanguvu kubwa za kiuchumi na kisiasa nchini Misri, pia litaongezewa jukumu la kusimamia mahakama ya uhalifu, iwapo kura hiyo itapitisha.

Kama suala hilo litapitishwa, marekebisho hayo yatampa rais madaraka zaidi na kuwepo kwa wanajeshi katika maeneo ya kijamii. Awamu ya urais itaongezwa kutoka miaka minne hadi sita na Sissi ataruhusiwa kugombania katika awamu ya tatu mwaka 2024.

Upigaji kura huo unafanyika chini ya wiki moja baada ya bunge la nchi hiyo kukubali mabadiliko hayo.

Wamisri ambao wanaishi nje ya nchi walianza kupiga kura siku ya Ijumaa.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa tatu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki. Zoezi hilo la upigaji kura litaendelea kwa muda wa siku tatu ili kuwawezesha wapiga kura kueleza msimamo wao.

Kituo cha televisheni ya taifa nchini Misri kimeripoti kuwa el-Sissi amepiga kura katika mkoa wa Heliopolis, karibu na kasri ya rais katika Jiji la Cairo.

Vyanzo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa sauti za upande wa upinzani zimenyamazishwa kwa jinsi ambavyo kura hiyo ya maoni ilivyokurupa kufanyika.

Vyombo vya habari vinavyounga mkono upande wa serikali vimekuwa vikifanya kampeni wiki kadhaa sasa na kuitaja "kura ya ndio kuwa ni wajibu wa kitaifa."

XS
SM
MD
LG