Janga la virusi vya corona limezorotesha diplomasia ya watu kushiriki binafsi katika mikutano ya Umoja wa Mataifa, Septemba mwaka jana bado ilikuwa ikionekana kuwa siyo salama kuwa na mikusanyiko ya kila mwaka ambapo takriban marais 200 na mawaziri wakuu na ujumbe wao mkubwa huhudhuria binfasi na hivyo mikutano hiyo ilifanyika kwa njia ya mitandao.
Chanjo zimefanya kuwa salama zaidi kufanya mikutano inayohudhuriwa na idadi ndogo ya watu, japokuwa kuenea kwa kasi kwa kirusi cha delta kulifanya wengi kuchelewesha maamuzi kuhusu kuhudhuria hadi dakika ya mwisho.
Viongozi pia wanahiari ya kubaki katika nchi zao na kutuma ujumbe wao kwa njia ya video, ambapo kiasi cha viongozi 50 wanapanga kufanya hivyo. Wengi kati yao ni viongozi wanaotoka katika nchi zenye kipato cha chini ambako chanjo zimekuwa na upungufu, ikionyesha ukosefu wa uwiano katika upatikanaji wa chanjo.
“Tunachohitaji ni mpango wa dunia wa chanjo, na tunahitaji wale wenye uwezo duniani kutumia nguvu zao kuleta usawa wa upatikanaji wa chanjo,” Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres amewaambia waandishi wa habari hivi karibuni.
Shirika la Afya Duniani limeweka lengo la kimataifa la kuwapatia chanjo angalau asilimia 40 ya watu katika kila nchi dhidi ya COVID-19 ifikapo mwisho wa mwaka huu, na asilimia 70 ya watu duniani ifikapo katikati ya mwaka 2022.
Zaidi ya dozi bilioni 5.7 za chanjo zimetolewa duniani, kiasi cha milioni 260 kupitia COVAX, juhudi ya kimataifa ya kusambaza kwa uwiano chanjo za COVID-19. Lakini nchi zenye kipato cha chini bado ziko nyuma ya zile tajiri, hususan za Afrika, ambako asilimia 2 tu ya dozi za chanjo za dunia zimetolewa.
Rais wa Marekani Joe Biden atakuwa na mkutano kwa njia ya mtandao Jumatano ambapo atasihi iwepo ni ya dhati kutoka kote sekta za umma na binafsi kufanya kazi kumaliza janga hili ikifikapo mwaka ujao.
“Tunajenga ushirikiano wa serikali, biashara na taasisi za kimataifa na asasi za kiraia kupanua uzalishaji wa chanjo, kuchochea fursa ya upatikanaji wa haraka zaidi wa chanjo na matibabu ya kuokoa maisha, na kuimarisha mifumo ya afya kote duniani,” Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas -Greenfield amewaambia waandishi wa habari Ijumaa.