Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 16:39

Marekani yakiri shambulizi la drone Kabul lilikuwa 'Kosa la Kuhuzunisha'


Jenerali Kenneth "Frank" McKenzie
Jenerali Kenneth "Frank" McKenzie

Shambulizi lililofanywa na ndege isiyokuwa na rubani yaani drone katika saa za mwisho za Marekani kuwaondoa watu Afghanistan halikumuua gaidi aliyekuwa anataka kuushambulia uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Kabul.

Lakini badala yake liliuwa takriban raia 10, akiwemo mfanyakazi wa misaada na watoto saba.

Kukiri huko Ijumaa kutoka kwa kamanda wa majeshi ya Marekani katika eneo kulifuatia uchunguzi uliochochewa na madai ya watu waliokuwa katika eneo, pamoja na ripoti za vyombo vya habari, kwamba shambulizi la kombora la Agosti 29 halikuwa ni tishio kabisa.

“Shambulizi lilitekelezwa kwa imani kwamba litazuia tishio la wazi kwa majeshi yetu na watu wanaohamishwa katika uwanja wa ndege,” Jenerali Kenneth “Frank” McKenzie, kamanda wa kikosi cha Central Command, aliwaambia waandishi wa habari huko Pentagon kwa njia ya video. “Uchunguzi wetu sasa unabainisha kuwa shambulizi hilo lilikuwa ni kosa kubwa.”

“Tumetathmini hivi sasa haiwezekani kwamba gari au wale waliokufa walikuwa wana uhusiano na kikundi cha ISIS-K,” McKenzie ameongeza, akitumia herufi za mkato za mshirika wa kikundi cha kigaidi cha Islamic State nchini Afghanistan, pia maarufu kama IS-Khorasan.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin pia aliomba radhi kwa shambulizi hilo la kimakosa.

“Kwa niaba ya wanaume na wanawake katika Wizara ya Ulinzi, salaam za dhati za rambi rambi kwa familia za wale waliouawa,” Austin alisema katika taarifa yake. “Tunaomba radhi, na tutajitahidi kujifunza kutokana na kosa hili la baya sana.

Msamaha ulikuwa ni mabadiliko makubwa kwa jeshi la Marekani, ambalo lilikuwa linatetea shambulizi la anga kwa wiki kadhaa.

Siku kadhaa ya tukio, Afisa wa jeshi wa ngazi ya juu zaidi wa jeshi la Marekani, Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi yote Jenerali Mark Milley, alitetea kuwa shambulizi hilo lilikuwa “sahihi.”

“Tunajua kutokana na njia nyingine mbalimbalii kuwa angalau mtu mmoja kati ya wale waliouawa alikuwa anawasaidia ISIS,” Milley aliwaambia waandishi wa habari wa Pentagon Septemba 1. “Taratibu zilifuatwa kwa usahihi.”

Hata wakati huo, habari kutoka eneo la shambulizi zilikuwa zinaeleza taarifa tofauti – kuwa badala ya kuuliwa msaidizi wa IS-Khorasan, ndege hiyo isiyo na rubani ilimlipua Ezmarai Ahmadi, mfanyakazi wa misaada wa taasisi ya Elimu na Lishe yenye makao yake California ambaye alikuwa amejiandikisha kuja kuhamia Marekani.

Wanafamilia wamesema wengine waliouliwa walikuwa ni binti yake Ahmadi, na wapwa zake wakiume na wike.

XS
SM
MD
LG