Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 22:28

Blinken kuzuru Qatar na Ujerumani kuendeleza diplomasia Afghanistan


 Antony Blinken
Antony Blinken

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken atazuru Qatar na Ujerumani wiki ijayo kufanya mazungumzo na washirika muhimu wa Marekani juu ya hali ya Afghanistan.

Blinken amewaambia waandishi wa habari Ijumaa katika Wizara ya Mambo ya Nje kuwa ataondoka Jumapili na ametoa “shukrani zake za dhati” kwa Qatar, kituo kikuu kwa usafirishaji kwa ndege wa idadi kubwa ya watu kutoka Kabul na kituo cha kwanza kupokea maelfu ya wakimbizi wa Afghanistan.

Mwanadiplomasia wa juu wa Marekani amesema baada ya hapo ataendelea na ziara yake kwenye kituo cha anga cha jeshi la Marekani cha huko Ramstein kilichopo kusini magharibi mwa Ujerumani, kuwashukuru wanajeshi wa Marekani na kukutana na wakimbizi wa Afghanistan.

Kadhalika Blinken amesema ataongoza mkutano kwa njia ya mtandao wa mawaziri kutoka mataifa 20 juu ya Afghanistan akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Mass. Amesema nchi hizo 20 “ zote zinajukumu la kusaidia kuwatafutia makazi Waafghanistan na kuhakikisha Taliban inatekeleza ahadi zao.”

Heiko Mass
Heiko Mass

Taliban wameahidi kuhakikisha usalama wa wale Waafghanistan na wengine wanaotaka kuondoka nchini humo, lakini Waafghanistan wengi wana mashaka uhakika wa ahadi hiyo walizotoa.

Katika matamashi yake Ijumaa, Blinken kwa mara nyingine ametetea kuondoka kwa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan, akisema kwamba ni idadi ndogo ya raia wa Marekani waliobaki nchini humo, na kuwa Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa ikiendelea kuwasiliana moja kwa moja na wote hao.

“Timu yetu mpya huko Doha inaendelea kulishughulikia suala hili,” amesema, na kila raia wa Marekani aliyebakia Afghanistan amepangiwa meneja wa kusimamia suala lake.

Wizara hiyo imewafikia raia wa Marekani waliobaki nchini Afghanistan mara 19 kabla ya wanajeshi wa Marekani wa mwisho kuondoka nchini humo wiki hii, na kuwa wengi kati yao wana uraia pacha na wakazi wa muda mrefu wa nchi hiyo ambao walikuwa wametatizika iwapo waondoke au wabakie.

Amesema Marekani bado ina nia ya dhati ya kumsaidia Mmarekani yeyote ambaye anataka kuondoka na kuwasaidia wale waliopewa Visa Maalum ya Uhamiaji na Waafghanistan wengine ambao walikuwa wakiisaidia Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema nchi yake inaendelea na mazungumzo na nchi zenye nguvu duniani kuanzisha tena safari za ndege za biashara kwenda Kabul. Kinacho subiriwa ni kuona iwapo mashirika yoyote ya ndege za biashara yatakuwa tayari kutoa huduma zake kwenda Kabul mara uwanja wa ndege utakapofunguliwa tena.

Blinken amewaambia waandishi wa habari ilikuwa muhimu mfumo wa uongozaji ndege za kiraia urudishwe na kusema kuwa Marekani ilikuwa imewafahamisha washirika wake taarifa juu ya kuanza huduma katika uwanja wa ndege wa Kabul.

FILE - Ndege ya kibiashara ikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamid Karzai, Kabul, Afghanistan, Agosti. 31, 2021.
FILE - Ndege ya kibiashara ikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamid Karzai, Kabul, Afghanistan, Agosti. 31, 2021.

Shirika la Ndege la Ariana la Afghanistan limeliiambia shirika la habari la AFP kuwa ndege zake zinazotoa huduma ndani ya nchi zimepangwa kurejesha huduma zake Ijumaa.

Kikundi cha mafundi kutoka Qatar na Uturuki kimekwenda Kabul Jumatano kusaidia kuufungua tena uwanja wa ndege, ambao ni kiungo muhimu kwa wale ambao bado wanataka kuondoka nchini au kupeleka misaada ya kibinadamu. Ndege ya mafundi hao ilikuwa ni ndege ya kwanza ya kigeni kutua uwanjani tangu uwanja kufungwa siku moja kabla bila ya sababu maalum.

Pia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ataitisha kikao kuhusu masuala ya kibinadamu cha ngazi ya mawaziri Septemba 12 huko Geneva kuzungumzia suala la kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu nchini Afghanistan, UN imetangaza Ijumaa.

Antonio Guterres a
Antonio Guterres a

Mkutano huo utashawishi kuongeza kwa haraka misaada ili operesheni za kibinadamu za kuokoa maisha ziweze kuendelea, na itaomba kikamilifu bila kizuizi ufikishaji wa misaada ya kibinadamu ili kuhakikisha Waafghanistan wanaendelea kupata huduma muhimu, UN imesema.

Takriban nusu ya watu wa Afghanistan milioni 38 wanahitaji misaada ya kibinadamu. Thekuthi moja ya Waafghanistan hawajui mlo waa wa pili utapatikanaje. Karibu nusu ya watoto wote walio chini ya miaka 5 wanatarajiwa kukabiliwa na hali mbaya ya utapiamlo katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Baadhi ya taarifa ya ripoti hii imetokana na vyanzo vifuatavyo The Associated Press, Agence France-Presse and Reuters.

XS
SM
MD
LG