Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 25, 2024 Local time: 03:45

NATO, G7 waanzisha uchunguzi wa mlipuko wa kombora nchini Poland lililotengenezwa Russia


Rais wa Marekani Joe Biden akiongoza mkutano wa dharura wa viongozi wa G20 huko Bali kujadili mlipuko uliotokea mashariki mwa Poland.
Rais wa Marekani Joe Biden akiongoza mkutano wa dharura wa viongozi wa G20 huko Bali kujadili mlipuko uliotokea mashariki mwa Poland.

Viongozi wa NATO na kundi la mataifa 7 walikutana kwa kikao cha dharura Jumatano asubuhi majira ya Indonesia pembeni ya mkutano wa viongozi wa G20 huko Bali kujadili mlipuko uliotokea mashariki mwa Poland.

Warsaw imeuhusisha shambulizi hilo na kombora lililotengenezwa Russia, kukiwa na uwezekano mkubwa wa kusambaa kwa vita vya Russia nchini Ukraine.

“Tumekubaliana kuiunga mkono Poland katika uchunguzi kuhusu mlipuko uliotokea katika eneo la vijijini la Poland karibu na mpaka wa Ukraine,” Rais wa Marekani Joe Biden aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano. “Nitahakikisha kuwa tunafahamu hasa kitu gani kilichotokea.”

Katika mkutano wa dharura ulioitishwa kwa haraka, Rais wa Marekani Joe Biden aliwakutanisha viongozi wa Canada, Tume ya Ulaya, Baraza la Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uholanzi, Uhispania na Uingereza kufuatilia mlipuko huo.

Biden alisema kwa hali ilivyo hivi sasa ilikuwa siyo rahisi kuwa kombora hilo lilirushwa kutoka Russia.

“Taarifa za awali zilizopo zinakinzana na hilo. Sitaki kusema hivyo mpaka uchunguzi wetu ukamilike,” aliongeza kusema.

Ugunduzi wa awali unaashiria kuwa kombora hilo lililopiga Poland lilirushwa na majeshi ya Ukraine kukabiliana na kombora la Russia lililokuwa likiwasili huko, kwa mujibu wa shirika la habari la AP, ambalo liliwanukuu maafisa wa Marekani.

Mwakilishi wa Moscow wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa mlipuko huo ulikusidiwa kuchochea vita kati ya Russia na NATO.

“Kuna jaribio la kuchochea vita vya moja kwa moja kati ya NATO na Russia, litakalopelekea maafa kwa ulimwengu mzima,” Dmitry Polyansky alisema katika taarifa iliyopachikwa katika mtandao wa Telegram.

Katika mkutano wao wa dharura Jumatano, viongozi pia walijadili mfululizo wa mashambulizi ya makombora ya Russia, Biden alisema, akiita vitendo vya Moscow “kwa jumla siyo vya busara.”

“Na wakati ulimwengu umekutana katika mkutano wa G-20 kuhimiza kuupunguza mgogoro huu, Russia inaendelea – imechagua kuzidisha mgogoro huu Ukraine. Wakati tunafanya mkutano huu,” Biden alisema.

XS
SM
MD
LG