Televisheni ya Russia ilionyesha video ya Putin akiangalia mazoezi hayo katika televisheni kubwa, huku kukiwa na maoni kutoka kwa viongozi wa kijeshi. Katika matangazo hayo, Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu alisema mazoezi hayo yalihusisha a nyambizi zenye kubeba silaha za nyuklia, ndege ya masafa marefu na mazoezi ya urushaji wa makombora ya balistiki na makombora ya masafa marefu.
White House ilisema Jumanne kuwa Russia ilikuwa imetoa taarifa kuwa itafanya mazoezi ya kila mwaka, yanayoitwa “Grom” au “Thunder.” Mazoezi hayo yamekuja wakati NATO imeanza mazoezi ya kila mwaka ya silaha za nyuklia, yajulikanayo kama “Steadfast Noon,” siku ya Jumatatu.
Kwa siku kadhaa, maafisa wa Russia walikuwa wanadai kuwa Ukraine inapanga kutengeneza na kutumia kile kiitwacho “bomu chafu” katika vita vyake na Russia.
Mabomu machafu yanatengenezwa kwa vilipuzi vya kawaida na malighafi zenye miale ya nyuklia ambayo yanaweza kusababisha vifo vya watu wengi na kuharibu mazingira.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejadili shutuma za Russia katika mkutano wa faragha Jumanne.
Ukraine na washirika wake wa Magharibi wamekanusha madai hayo kwa nguvu zote na wanadhani wanatumika kama chambo cha aina fulani cha kukuza vita huko Ukraine.
Akizungumza kutoka makao makuu ya ushirika huo mjini Brussels Jumatano, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameziita tuhuma hizo “upuuzi” na “uongo wa dhahiri,” na kuionya Russia kutotumia kisingizio cha uongo kukuza vita hivyo.
Rais wa Marekani Joe Biden ametoa onyo kama hilo Jumanne. Alipoulizwa na waandishi iwapo alifikiria Russia ilikuwa inatumia kisingizio cha bomu chafu kuweka ishara ya uongo ya operesheni na kutumia bomu lake chafu, alisema, “Russia itakuwa inafanya kosa la kustaajabisha ikiwa itatumia mbinu ya silaha za nyuklia.”
Mwandishi wa UN amechangia katika habari hii.