Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 22:35

Kimbunga Kenneth chasababisha vifo vya watu 38 Msumbiji


Athari zilizoletwa na kimbunga Kenneth katika Wilaya ya Macomia, Jimbo la Cabo Delgado, Msumbiji, Aprili 27, 2019.
Athari zilizoletwa na kimbunga Kenneth katika Wilaya ya Macomia, Jimbo la Cabo Delgado, Msumbiji, Aprili 27, 2019.

Watu 38 wamethibitishwa kuwa wamepoteza maisha nchini Msumbiji kutokana na janga la kimbunga Kenneth, kimbunga cha pili hatarishi kilichopiga nchi hiyo baada ya wiki sita.

Taasisi ya usimamizi wa majanga Msumbiji imesema Jumatatu idadi ya vifo, ambayo awali ilikuwa ni watu wasiopungua watano, imeongezeka wakati nchi hiyo ikisubiri mvua nyingi zaidi.

“Mvua imekuwa inanyesha kwa nguvu tangu Jumapili asubuhi,” amesema Deborah Nguyen, msemaji wa Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa.

“Tunawasiwasi mkubwa kwa sababu, kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa, mvua kubwa zinatarajiwa kuendelea siku nne zijazo.”

Mvua hizo zimesababisha mafuriko na maporomoko, na mvua zaidi zitaongeza mashaka, kuharibu barabara ambazo makundi yanayotowa misaada yanazitumia kusafirisha mahitaji muhimu yakiwemo madawa na vyakula.

Takriban watu 200,000 wako hatarini upande wa kaskazini mwa Jiji la Pemba.

Taasisi ya taifa ya kusimamia maafa Msumbiji imesema Jumapili zaidi ya watu 23,000 hawana makazi ya kuishi na makazi 35,000 yemaharibiwa au kuangamia.

Kabla ya kimbunga hicho kuwasili Msumbiji, Kenneth ilipita katika kisiwa cha Comoros na kuua watu watatu.

Siku ya Jumapili, UN ilitoa dola za Marekani milioni 13 kusaidia chakula, makazi, madawa, maji na udhibiti wa maji taka kuwasaidia watu walioathiriwa na kimbunga Kenneth.

Kimbunga Idai kilipiga upande wa kusini mwa Afrika mwezi Machi na kuua zaidi ya watu 1,000 nchini Msumbiji, Zimbabwe, Malawi na Madagascar.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG