Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 12:39

Kimbunga Idai : Serikali ya Zimbabwe yapeleka maombi kwa jumuiya ya kimataifa, idadi ya vifo ni zaidi ya watu 600


Rais Emmerson Mnangagwa akizungumza na waathirika wa janga la kimbunga Idai
Rais Emmerson Mnangagwa akizungumza na waathirika wa janga la kimbunga Idai

Serikali ya Zimbabwe imesema imepeleka maombi kwa jumuiya ya kimataifa ipatiwe msaada wa madawa, chakula na ujenzi wa miundombinu, wakati waathirika wa kimbunga Idai wakishinikiza misaada hiyo kutumwa haraka iwezekanavyo. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wahanga wa janga hilo wamefikia 615.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Ujerumani inaripoti kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la uratibu wa misaada ya kiutu, OCHA, limesema watu 417 wamepoteza maisha Msumbiji,139 Zimbabwe na 59 Malawi.

Vyombo vya habari vinaeleza kuwa baba wa Better Mungana alikufa na ndugu yake alipotea wakati kimbunga kilipopiga Zimbabwe, Malawi na Mozambique wiki iliyopita.

Mungana, ambaye anaishi katika Jiji la Chimanimani lililoathirika vibaya sana na kimbunga, anataka serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa kumsaidia yeye na familia yake.

“Tangu Kimbunga Idai kupiga eneo hilo, tunahangaika kupata chakula, nguo zetu zilichukuliwa na maji, na hivi sasa hatujui cha kufanya,” amesema.

“Serikali imeahidi kutusaidia kwa kutupa hifadhi ya mahali pakuishi, lakini inaelekea kuwa msaada huo utakwenda hata kwa watu ambao hawakuathiriwa na mafuriko. Nimempoteza baba yangu, na bado tunamtafuta ndugu yangu. Inauma sana. Hatuna chakula wala makazi.”

Mwili wa ndugu yake ulipatikana Ijumaa jioni na kuzikwa, lakini chakula na makazi bado ni tatizo.

Hali hiyo pia inaikabili familia ya Dube-Magoso iliyoko mita 500 kutoka eneo hilo. Baba yao mwenye umri wa miaka 83 alikufa wakati nyumba yao ilipobomoka wakati wa kimbunga hicho ; mama yao alinusurika lakini alipata majeraha kadhaa.

Mtoto wao, Musavengana Dube Magoso, anasema wanataka serikali ya Zimbabwe kuwasaidia.

“Serikali lazima itutafutie sehemu bora ya kwenda kuishi ili tuweze kufanya kazi kupata kipato chetu ili sote tuweze kupata njia ya kuendesha maisha yetu,” amesema. “Hadi hivi sasa, hatuna chakula – kile tulichokuwa tumepanda kwa ajili ya chakula chetu kimeharibiwa na maji. Tumerudishwa nyuma kabisa kimaisha.”

Wafanyakazi wa dharura wameeleza mafuriko hayo yaliyofuatia kimbunga Idai kama ni janga kubwa kuliko yote katika kipinidi cha miaka 20.

Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa hata hivyo, bado nchi hizo zinaendelea kuwatafuta wananchi wake waliopotea na huenda taarifa kutoka kwenye maeneo yaliyokumbwa na kimbunga hicho kibaya kilichosababisha mafuriko, zikaongeza idadi ya wahanga wa mafuriko hayo.

Umoja wa Mataifa tayari umeongeza kiwango cha msaada wa dharura na limeonya kuhusu uwezekano wa milipuko ya magonjwa.

Nchi hizo tatu za Kusini Mashariki mwa Africa tayari ziko katika uangalizi wa Umoja wa Mataifa sawa na zile zinazohitaji misaada ya dharura kama vile Yemen, Sudan na Syria.

XS
SM
MD
LG