Serikali ya Marekani imekuwa inataka Chang akabidhiwe kwao kujibu madai ya jinai ya kifedha, kwa mujibu wa afisa wa Afrika Kusini.
Chang, 63, amepangiwa kesi hiyo ya kurudishwa Msumbiji isikilizwe Jumanne huko Johannesburg.
Amekuwa akizuiliwa nchini humo tangu alipokamatwa Disemba 29 alipokuwa akijiandaa kwenda Dubai.
Anakabiliwa na mvutano ulioko kati ya Marekani na Msumbiji ambapo pande zote zinamtaka apelekwe katika nchi hizo kwa madai ya kuhusika kwake na kashfa ya mkopo wa siri wa dola bilioni 2 ambao ulikaribia kuifilisi Msumbiji na kuwaweka mtegoni sio chini ya watu 18 katika pande zote mbili za bahari ya Atlantic.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Lindiwe Sisulu, ameliambia gazeti la Daily Maverick katika mahojiano yaliyochapishwa Alhamisi kuwa serikali yake ilikuwa imekubali kumkabidhi Chang Mozambique kukabili mashtaka dhidi yake.
“Sisi tunampeleka Msumbiji akajibu mashtaka. ….Na tunaamini hilo ni jepesi zaidi kwa kila mtu,” amesema.
Wasaidizi wa mahakama wanaoamua iwapo ipo kesi ya jinai dhidi ya mtuhumiwa, Disemba 19 walimtuhumu Chang na wengine sita kwa kosa la utakatishaji fedha, wizi na hongo.
Wanasema watu hao walikuwa wametengeneza miradi ya baharini ya uongo, ikiwemo chombo cha kuvulia samaki aina ya tuna na meli za doria zilizotakiwa kufanya ulinzi wa eneo pana la pwani ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Serikali ya Msumbiji imemtuhumu Chang kwa ubadhirifu wa fedha zenye kiwango kisichopungua dola milioni 12 wakati akiwa waziri wa fedha, kuanzia mwaka 2005-2015.
Dola bilioni 2 za mikopo ya siri ilikuja kujulikana baada ya ukaguzi wa mahesabu uliofanyika 2016. Lakini Chang anakanusha kuhusika na makosa hayo.